MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa mwito kwa mataifa duniani kuungana katika kutoa mchango kwa Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) ufikie lengo la kukusanya dola za Marekani bilioni 18.
Dk Mpango alisema hayo Jumatano jijini New York nchini Marekani alipohutubia Mkutano wa Saba wa kuiwezesha Global Fund.
Katika mkutano huo, Tanzania imeahidi kuchangia dola za Marekani milioni moja (Sh bilioni 2.3) katika Global Fund ili kuuwezesha kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Dk Mpango alisema migogoro imepunguza juhudi za kurejesha uchumi wa nchi nyingi ulioathirika na janga la Covid-19 na kuongeza changamoto katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Alisema Tanzania inathamini ushirikiano wa kihistoria uliopo baina yake na Global Fund ambao umekuwa na matokeo chanya na kuwezesha kupunguza idadi ya vifo kwa Ukimwi, kifua kikuu na malaria.
Aliishukuru Bodi ya Global Fund kwa kuiunga mkono Tanzania kwa miaka mingi, na akazishukuru na kuzipongeza serikali, mashirika, taasisi na watu binafsi kwa michango yao kwa mfuko huo kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Dk Mpango alisema Tanzania imejitolea kufikia lengo la kimataifa la kukomesha Ukimwi ifikapo 2030 kwa kutumia teknolojia mpya na mikakati ya kibunifu.
Alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kukabili Ukimwi, kifua kikuu na malaria, bado Tanzania inakabiliwa na changamoto ya maambukizi mapya hasa kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24.
Pia alisema katika kukabili kifua kikuu bado taifa linakabiliwa na vikwazo ukiwamo upatikanaji mdogo wa huduma za uchunguzi wa ugonjwa huo hasa katika maeneo yenye watu walio hatarini wakiwamo na wafanyakazi wa migodini, wavuvi na wafungwa.