Tanzania kuvuna bil 663/- za mahindi

DAR ES SALAAM – WIZARA ya Kilimo imesema uamuzi wa Tanzania kuuza tani 650,000 za mahindi nchini Zambia ni fursa kwa wasafi rishaji.

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alieleza jana kuwa Tanzania itapata dola za Marekani milioni 250 sawa na Sh bilioni 663 kwa kuuza mahindi nchini Zambia.

“Timu ya Tanzania na Zambia itakaa chini kujadili logistiki za usafirishaji, tukiwa na lengo la kuyapa makampuni ya Tanzania na Zambia kipaumbele kushiriki kikamilifu kwenye fursa hii,”alieleza Bashe.

Advertisement

Alieleza kuwa kutokana na ukame unaoikumba nchi hiyo imesaini makubaliano ya kununua tani 650,000 za mahindi Tanzania kuwasaidia wananchi milioni saba wa taifa hilo.

Bashe alieleza kuwa mkataba huo ulisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala ya Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Dk Andrew Komba na Mratibu wa Maafa kitaifa nchini Zambia, Dk Gabriel Pollen. Alieleza kuwa yeye, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Kilimo Zambia, Reuben Phiri walishuhudia tukio la kusainiwa kwa mkataba huo.

SOMA: Majaliwa ataka mpango kuwezesha waraibu

Bashe alieleza kuwa mkataba huo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi minane na mahindi hayo yatakayosafirishwa kwenda Zambia yatatolewa katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA). “Kituo cha Songwe kitatoa tani 55,000, Makambako tani 75,000, Sumbawanga tani 250,000 na Songea tani 270,000,” alieleza.

Aliongeza: “Sambamba na Zambia kununua tani 650,000 za mahindi kutoka Tanzania, pia tumeingia mkataba wa kuuza Tani 500,000 za mahindi kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC) na mkataba wa kuuza tani 100,000 za unga wa mahindi WFP (Mpango wa Chakula Duniani)… Tanzania inaendelea kutekeleza mkataba na WFP wa kuuza unga nchini Malawi”.

Mei mwaka huu NFRA ilisaini mkataba wa kuuza tani 500,000 za mahindi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). NFRA na kampuni ya Quincy ya DRC walisaini mkataba huo kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Katanga wanaokabiliwa na njaa.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli alisema Dodoma kuwa kwa kuzingatia mkataba huo katika awamu ya kwanza watanunua tani 200,000 na awamu ya pili watanunua tani 300,000. Mweli alisema wameanza ushirikiano wa biashara ya mazao kama moja ya mkakati waliouweka kwa ajili ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula nchini na bara la Afrika kwa ujumla.

Alisema kuna akiba ya chakula katika maghala nchini na tayari wamefungua vituo 14 vya kukusanyia mazao na kwamba ajenda ni kujilisha wenyewe na kufanya biashara. Mweli alisema serikali imetenga Sh bilioni 300 kwa ajili ya uwekezaji wa kununua mazao ya chakula tani 300,000 na msimu unapoanza NFRA itaanza ukusanyaji wa mazao ya chakula.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa NFRA, Dk Komba alisema msimu wa unaonza leo (Julai Mosi) wanaanza ukusanyaji wa mazao ya chakula yakiwemo mahindi, mpunga na mazao mengine. Bashe alieleza kuwa Julai 10, mwaka huu NFRA itaanza kununua mahindi na sasa imeanza kusaini mikataba ya wasambazaji wa Tanzania.

Alieleza kuwa mikataba hiyo inatekelezwa na NFRA kwa kushirikiana na Bodi ya Chakula na Mazao Mchanganyiko (CPB). “Niwahakikishe wakulima wote wa mahindi, bei ya NFRA itatangazwa na itakua wazi, NFRA itanunua mahindi kwa zaidi ya shilingi 500/kilo,”alieleza.