Tanzania, Misri kushirikiana ukarabati wa barabara

WIZARA ya Ujenzi kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi nchini Misri zimekubaliana kushirikiana kukarabati barabara ya kimkakati ya kutoka Cairo Misri hadi Capetown itakayosaidia kufungua fursa za uchumi nchini .

Imesema utekelezaji wa makubaliano hayo yatawezesha pia kuunganisha na nchi nyingine za Afrika na kwamba mazungumzo yameanza.

Waziri wa Ujenzi nchini, Innocent Bashungwa amesema hayo leo Dar es Salaam baada ya kufanya majadiliano na Waziri wa Uchukuzi wa Misri Kamel al-Waziri aliyefika nchini kwa ajili ya kuona fursa za ushirikiano zilizopo nchini pamoja na kujifunza.

Advertisement

Akizungumza Bashungwa amesema mjadala huo na ujumbe kutoka Misri ni moja ya jitihada za kuendelea kufungua nchi na kuimarisha mahusiano kati ya nchi ya Tanzania na nchi mbalimbali.

‘Wenzetu kutoka Misri wametembelea Tanzania kujadiliana namna ya kushirikiana kimkakati kama mnavyofahamu kuna barabara ya Cairo- Misri hadi Capetown ambapo ni moja ya mjadala tumejadili kuona ni namna gani tutashirikiana kuimairsha mtandao huo wa barabara kwani kipande cha barabara hiyo kimepita hapa nchini,” amesema.

Amesema kipande hicho cha barabara kwa Tanzania kina ukubwa wa kilomita 1600 kikianzia upande wa nyanda za juu kusini kinapita katika mikoa ya Songwe, Mbeya, Iringa, Dodoma, Manyara, Arusha na Namanga kuelekea Kenya.

Bashungwa amesema hivyo moja ya vitu walivyokubaliana kati ya Wizara hizo ni kuona kwa pamoja namna ya ushirikiano kukarabati kipande hicho cha barabara na jambo hilo lifanywe kwa haraka kwa kuwa litasaidia kuwezesha kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwa kukua kwa uchumi lazima kuendane na ubora wa barabara.

Aidha amesema katika majadiliano hayo wamejadili namna ya kushirikiana ili vijana wahandisi wanaomaliza vyuo kutatua changamoto zinazowakabili na kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa nchini ili washiriki vijana wazawa.

‘Tayari tumeijulisha Tanroads (wakala wa barabara Tanzania ) ili kuweka vigezo vitakavyolazimisha wenye miradi kuwatumia vijana kwamba katika kilomita fulani iwepo idadi kadhaa ya vijana,” amesema lengo la kufanya hivyo nikusaidia kundi hilo.

Kadhalika amesema wamejadili namna ya kuendelea kubadilishana uzoefu kwa kupitia taasisi za Wakala wa Majengo (TBA) ili waende wakajifunze kutoka Misri wapate uzoefu katika ujenzi wao hivyohivyo kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) jambo litakalosaidia wakandarasi wazawa.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mohamed Besta amesemaTanzania ina mtandao wa kilomita 4321 za barabara ambazo hazijajengwa kwa kiwango cha lami na kwamba kupitia mfumo wa ushirikishwaji wa sekta binafsi (PPP) ndio eneo wanalohitaji ushirikiano ili ziweze kukamilika ifikapo mwaka 2026.

Amesema kwa ujumla Tanzania ina mtandao wa barabara wa kilomita 181,655.49.

Kwa upande wake Kamel al-Waziri amempompongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu ujumbe huo kufika nchini ili kujifunza kuzijua fursa mbalimbali zilizopo na kushirikiana kujenga nchi katika Nyanja mbalimbali.

Amesema nchi ya Misri ina wabobevu wa eneo la ujenzi wa barabara na hata chuo kikuu cha ujenzi maeneo ambayo kwa ujumla wake wakishirikiana na Tanzania yanaweza kuleta tija.

Kuhusu barabara ya Cairo-Misri hadi Capetown amesema ni muhimu kuiunganisha barabara hiyo ili kuwezesha usafiri kwa nchi mbalimbali za Afrika .