Tanzania, Qatar wajadili nafasi za ajira

MAWAKALA wa ajira katika sekta binafsi nchini wamekutana na kujadili fursa za ajira na mawakala wenzao wa ajira binafsi wa Qatar, jijini Doha.

Mawakala hao wameongozana na Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Profesa Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab.

Ujumbe wa Chemba ya Biashara ya Qatar ukizungumza na Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab Jijini Doha tarehe 30 Agosti, 2022

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Kitengo cha Uratibu kutoka Wizara ya Kazi nchini Qatar, Hamad Ali Elfaifa alisema Qatar na Tanzania zina uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria ambao umedumu hadi sasa na wanapenda kuuendeleza kwa kushirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya ajira.

Advertisement

Elfaifa aliwataka mawakala wa ajira kutoka Tanzania kuzingatia sheria na taratibu za ajira pamoja na kushirikiana na mawakala wenzao wa Qatar ili kupata wafanyakazi wenye ujuzi, maarifa na weledi kwa maslahi ya pande zote mbili.

Alisema katika kutekeleza mkataba wa ajira kati ya Tanzania na Qatar, Tanzania imeingizwa kwenye mfumo wa ajira nchini Qatar ambapo mawakala watapokea maombi ya kazi kutoka kwa mawakala wa Qatar, hatua itakayowezesha Watanzania wengi wenye sifa kunufaika na nafasi za kazi nchini Qatar.

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe wa Serikali ya Tanzania, Profesa Katundu alisema Tanzania inajivunia kuwa na vijana wenye ujuzi na uzoefu katika fani mbalimbali hivyo wanaamini kuwa endapo vijana hao watapatiwa fursa za ajira nchini Qatar watasaidia kuboresha zaidi uchumi wa Qatar pamoja na maisha yao.

Naye, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira (TaESA), Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Joseph Nganga alisema lengo la kuwakutanisha mawakala wa ajira binafsi wa Tanzania na wa Qatar ni kufahamishana taratibu za ajira kwa pande zote mbili ili kufanya kazi kwa ushirikiano na kupata waajiriwa wenye sifa stahiki.

Mwaka 2014 Tanzania ilisaini mkataba wa makubaliano ya ajira na Qatar, ambapo kwa sasa serikali inaangalia namna ya kupata nafasi za ajira kwa Watanzania ili waende kufanya kazi nchini humo.

 

 

 

 

 

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *