TANZANIA na Taasisi ya WorldFish kutoka Malaysia wamekubaliana kushirikiana kuimarisha sekta ya uvuvi ili kuwa na mchango mkubwa nchini sambamba na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Hatua hiyo imekuja baada ya leo Disemba 4, 2023 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu, Essam Yassin Mohammed wa Taasisi ya Utafiti na Ubunifu katika minyororo ya thamani ya uvuvi na ukuzaji viumbe (Worldfish) katika Mkutano wa COP 28, Dubai, UAE.
Aidha, pamoja mambo mengine, wamekubaliana kuhakikisha taasisi hiyo inaweka nguvu katika afua za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo uoteshaji wa matumbawe, kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa, kukuza ukuzaji viumbe maji bahari na kuboresha kosaafu za viumbe maji wakuzwao huku akimkaribisha kufungua ofisi ya WordFish nchini Tanzania.