Tanzania, Uganda kuimarisha ushirikiano sekta mbalimbali

DAR ES SALAAM; KATIKA jitihada za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kukuza maendeleo ya pamoja ukanda wa Afrika Mashariki, serikali za Tanzania na Uganda zimeanza majadiliano ya pamoja yanayolenga kuimarisha ushirikiano wa sekta mbalimbali ikiwemo siasa, elimu, uchumi, biashara na kilimo.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kufungua fursa mpya za maendeleo na kuongeza ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili jirani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 12, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Mashariki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ali Bujiku, amesema majadiliano hayo yalianza rasmi Machi 11 na yanatarajiwa kuendelea hadi Machi 13 mwaka huu.

Balozi Bujiku amesema mkutano huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kikanda pamoja na kufuatilia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wakuu wa nchi hizo mbili.

Amesema majadiliano hayo yataweka msingi wa utekelezaji wa miradi na sera zinazolenga kukuza maendeleo ya pamoja kati ya Tanzania na Uganda.

“Majadiliano haya yanalenga kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali na kuhakikisha maelekezo yaliyotolewa na viongozi wakuu wa nchi hizi mbili yanaanza kutekelezwa kwa vitendo,” amesema Bujiku.

Aidha, amesema katika mkutano huo pande hizo mbili zinalenga kufikia maazimio manne muhimu yatakayosaidia kuanza rasmi utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa Tanzania na Uganda katika maeneo ya kipaumbele.

“Tutajadili kwa kina namna ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja za siasa, uchumi, biashara pamoja na kilimo ili kuhakikisha mataifa yetu yanaendelea kunufaika na fursa zilizopo katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button