TANZANIA itakuwa kitovu cha maunganisho ya mawasiliano Afrika Mashariki na Kati kutokana na kuwapo kwa mkongo wa mawasiliano wa pili barani Afrika utakaokamilika Februari mwakani.
Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Jim Yonazi alisema hayo alipofanya ukaguzi wa mkongo wa kituo cha 2 Afrika jana na kueleza kuwa hilo linafanyika kutokana na juhudi za serikali kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha maunganisho ya mawasiliano.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho una faida kubwa kwa nchi kwa kupata mtandao wa intaneti wenye kasi zaidi na uhakika wa kuunganishwa duniani.
“Mkongo unaokuja unapitia Kusini mwa Bara la Afrika, kwa hiyo tutapata uhakika wa maunganisho kwenda duniani na kusaidia sana biashara ya kuuza uwezo nchini mwetu na nchi jirani na kuwasaidia wananchi wetu na nchi jirani kuweza kushiriki katika uchumi wa kidijitali ambao ndio uchumi sasa dunia inashiriki,” alisema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Airtel Tanzania, Beatrice Singano alisema wanatengeneza eneo la kusambaza mawasiliano yanayopitia baharini kuiwezesha Tanzania kufikiwa na kufikia maeneo mengine kimawasiliano.
Kituo cha Mkongo wa 2 Africa Submarine kinatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2023 kwa kufika katika zaidi ya maeneo 35 katika nchi 26 duniani.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed akifunga mkutano wa nne wa Connect to Connect ‘C2C’ Dar es Salaam, alisema nchi imeshasimika miundombinu ya mawasiliano ya simu na mkongo kuwezesha huduma za mawasiliano ya Tehama kwa nchi jirani.
Alitaja nchi hizo ni Rwanda, Burundi, Msumbiji, Zambia, Malawi na Kenya hatua itakayoifanya nchi kuwa kitovu cha tehama cha kutegemewa kwa muunganisho wa mawasiliano ya haraka ya intaneti.
Alisema Tanzania imejipanga kuwa kitovu cha Tehama kupitia utekelezaji wa miradi kama vile Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Mfumo wa kidijiti wenye kanzidata ya anuani za makazi (NaPA).
“Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) karibu itapokea huduma hizo za teknolojia ya habari na mawasiliano,” alisema Mohamed wakati akifunga mkutano wa nne wa Connect to Connect ‘C2C’ 2022 uliofanyika Dar es Salaam.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema mkutano huo unaunga mkono ajenda ya kidijiti ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuleta mseto wa uchumi wa nchi, pamoja na kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi katika kupata huduma ya mawasiliano na kwa gharama nafuu.