Tanzania yamtunuku heshima Rais wa AfDB

TANZANIA imetambua mchango wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinwumi Adesina katika maendeleo nchini na kumtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Sayansi (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Pia, serikali imeishukuru AfDB kwa mchango wake katika kuleta mageuzi ya kilimo na maendeleo ya kiuchumi, sekta ya fedha na miundombinu nchini.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais mstaafu Jakaya Kikwete amemtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Sayansi, Dk Adesina kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya uchumi nchini na Afrika kwa ujumla, wakati wa Mahafali ya 55 ya chuo hicho yaliyofanyika jana mkoani Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema kutunukiwa kwa shahada hiyo kunaakisi uongozi bora wa Dk Adesina ulioshuhudiwa na watu duniani katika kuchochea maendeleo na kuboresha miundombinu na kukuza uchumi.

“Tanzania inajivunia uongozi wake kupitia Mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora uliofadhiliwa na AfDB chini ya Dk Adesina, uliwezesha vijana wa Kitanzania zaidi ya 11,000 kupata mitaji na kujiendeleza katika eneo la
kilimo biashara,” alisema Dk Mwigulu.

Pia, alizungumzia mchango wa AfDB na Benki ya Dunia katika mkakati wa kusambaza umeme Afrika kupitia Mkutano wa Nishati Afrika uliofanyika nchini Januari 27 na 28, mwaka huu kama moja ya vitu vilivyompa ushawishi mkubwa Afrika.

Alisema Dk Adesina amekuwa miongoni mwa watu wanaopaza sauti za Waafrika kimataifa katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula na usawa katika ushirikiano kibiashara.

Aidha, alisema Dk Adesina ameiongoza AfDB katika kufadhili miradi ya kimkakati yenye manufaa kwa wananchi wa kawaida na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora – Kigoma hadi Burundi na Congo, Kiwanja cha Ndege cha Msalato na barabara za Mzunguko Dodoma zinazounganisha makao makuu ya nchi na mikoa jirani.

Akisoma wasifu wa Dk Adesina, Profesa Rwekeza Mukandala alisema UDSM inatambua mchango wa Dk Adesina katika kukuza uchumi na kumtunuku shahada hiyo.

“Chini ya uongozi wake, AfDB iliongeza mtaji wake kwa kiwango kikubwa katika historia yake wanahisa walipandisha mtaji wa jumla kutoka Dola za Marekani bilioni 93 mwaka 2015 hadi bilioni 208 mwaka 2019,” alieleza Profesa Mukandala.

Alisema kupitia vipaumbele vya Dk Adesina vya kuiangaza Afrika, kuilisha Afrika, kukuza viwanda, kuiunganisha Afrika na kuboresha maisha ya Waafrika, vimeleta matokeo chanya kwa Waafrika zaidi ya milioni 500.

Alisema AfDB chini ya uongozi wake imekuwa kinara katika uwekezaji kwenye miundombinu ikiwekeza dola za Marekani bilioni 55 katika miradi ya miundombinu.

Kwa upande wa Tanzania, Profesa Mukandala alisema AfDB ilipitisha mkakati wa kuboresha maisha ya Watanzania na kuendeleza ushirikiano wa kikanda.

Mkakati huo ulijikita katika kuchochea miundombinu endelevu kwa uchumi shindani na mazingira bora kwa sekta binafsi ili kuongeza ajira.

“Benki imekuwa mstari wa mbele katika kuleta mageuzi ya kilimo hatua iliyowezesha Tanzania kufikia asilimia 128 ya utoshelevu wa chakula. Kupitia uongozi wake Dk Adesina ameonesha dhamira ya kutatua changamoto za kilimo Afrika,” alisisitiza.

Dk Adesina ambaye anamalizia muda wake wa uongozi, yuko nchini kwa ziara rasmi kuanzia Juni 12 hadi 15, mwaka huu. Leo anatarajiwa kutembelea miradi kadhaa inayofadhiliwa na benki hiyo nchini mkoani Dodoma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button