Tanzania yanadi fursa za uwekezaji mnyororo madini muhimu London

TANZANIA imeendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha maendeleo ya Sekta ya Madini barani Afrika, kwa kuelezea mikakati madhubuti ya kuendeleza madini muhimu na mkakati yanayopatikana nchini.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema hayo wakati akihutubia Mkutano wa kimataifa wa Uwekezaji katika Mnyororo wa Thamani Madini Muhimu nchini Tanzania (Investing in Tanzania’s Minerals Value Chain) unaofanyika jijini London, Uingereza.
SOMA: Tanzania, Uingereza kushirikiana kuendeleza madini mkakati
Mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa madini muhimu, uliwakutanisha Wawekezaji wa Kimataifa, Watunga Sera, Wataalam wa Sekta ya Madini, na Wawakilishi wa mashirika ya maendeleo kutoka pande mbalimbali za dunia.
Mbibo ameeleza malengo ya Tanzania ya kuimarisha Sekta ya Madini kupitia ushirikiano wa kimataifa, teknolojia bunifu, na uendelezaji wa mnyororo wa thamani wa madini kwa njia endelevu.
Ameongeza kuwa, Tanzania ina fursa lukuki zinazopatikana nchini katika maeneo ya utafiti wa madini, uongezaji thamani kwa kutumia viwanda vya ndani, pamoja na usimamizi shirikishi unaojali mazingira na maslahi ya wananchi.
Amesisitiza kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na madini muhimu kama Nikeli, Kobalti, Lithiamu, Shaba, Kinywe (Graphite), na madini adimu (Rare Earths Elements – REEs), ambayo ni nguzo muhimu katika mapinduzi ya nishati safi duniani.
Aidha, Mbibo amesisitiza kuwa, Serikali ya Tanzania imeweka mikakati thabiti ili kuhakikisha madini hayo yananufaisha taifa.
Ameitaja mikakati hiyo kuwa ni kuimarisha uwekezaji katika utafiti na uchimbaji endelevu, kukuza viwanda vya kuongeza thamani madini ndani ya nchi, kuongeza uwazi katika mnyororo wa madini, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa unaozingatia Sera za kitaifa, na kuboreshwa kwa uwezo wa taasisi zinasimamia Sekta ya Madini.
Mbibo ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuratibu mkutano huo muhimu, na kumpongeza Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Young, kwa mchango wake katika kuimarisha ushirikiano wa pande mbili za mataifa hayo.