Safari ya Tanzania Kuelekea Uchumi wa Kidijitali

Kutoka minara ya mawasiliano na Mkongo wa Taifa hadi ajira za mtandaoni, biashara za kidijitali na ubunifu wa vijana, Tanzania inaingia katika enzi mpya ambapo internet si tena chombo cha mawasiliano pekee bali injini ya uchumi, ungana na Sylivestre Domasa kwenye makala haya:

Kila asubuhi, Baraka Mafole huwasha kompyuta yake na kuanza kazi na wateja waliopo maelfu ya kilomita kutoka Tanzania.

Mmoja anaweza kuwa nchini Marekani, mwingine Canada na mwingine Ulaya. Wengi wao hajawahi kukutana nao ana kwa ana.

Kinachowaunganisha ni internet.

Kupitia ujuzi wake wa lugha ya Kiswahili na majukwaa ya kidijitali, Mafole anasema ameweza kuingiza zaidi ya dola 10,000 akifanya kazi mtandaoni. Miaka michache iliyopita, fursa kama hiyo ilikuwa ngumu kufikirika kwa vijana wengi wa Tanzania.

Leo, hadithi yake ni sehemu ya mabadiliko makubwa yanayoendelea nchini; mabadiliko yanayobadilisha internet kutoka chombo cha mawasiliano kuwa chombo cha uzalishaji, biashara na ajira.

Lakini safari hiyo haikuanza kwa bahati mbaya.

Kutoka Ahadi Hadi Mapinduzi ya Kidijitali

Mwaka 2022, Serikali ilitangaza rasmi kuwa Tanzania ilikuwa ikiingia katika kile kilichoelezwa kama Mapinduzi ya Kidijitali.

Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Waziri wa wakati huo, Nape Nnauye, alieleza kuwa sekta hiyo ilikuwa imepewa jukumu la kuweka msingi wa uchumi wa kidijitali kupitia upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano, matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa internet kwa wananchi wengi zaidi.

Miaka minne baadaye, takwimu zinaonesha mabadiliko hayo yanaanza kuonekana.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, watumiaji wa intaneti nchini waliongezeka kutoka milioni 49.3 Machi 2025 hadi milioni 58.9 Machi 2026, sawa na ongezeko la asilimia 19.5 ndani ya mwaka mmoja.

Katika kipindi hicho, watumiaji wa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu waliongezeka kutoka milioni 66.5 hadi milioni 81.0 huku laini za simu zikiongezeka kutoka milioni 90.4 hadi milioni 111.9.

Aidha, idadi ya watoa huduma za miundombinu ya mawasiliano iliongezeka kutoka 38 hadi 52 katika kipindi hicho.

Kwa wachumi wa maendeleo, takwimu hizo si za mawasiliano pekee. Ni viashiria vya uchumi unaozidi kuwa wa kidijitali.

Minara 758 na Tanzania Mpya ya Kidijitali

Wakati Mafole akifanya kazi na wateja wa kimataifa kupitia internet, msingi wa mafanikio hayo ulianza mamia ya kilomita kutoka mijini.

Kwa miaka mingi, maeneo mengi ya vijijini hayakuwa na mvuto wa kibiashara kwa kampuni za mawasiliano kutokana na gharama kubwa za uwekezaji.

Matokeo yake, maelfu ya wananchi waliishi bila huduma za mawasiliano za uhakika.

Ili kuziba pengo hilo, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliendelea kutekeleza miradi ya kuongeza upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo ambayo hayakuwa yakihudumiwa na kampuni za simu kwa kiwango cha kutosha.

Matokeo ya juhudi hizo ni ujenzi wa minara 758 katika kata 713 nchini.

Minara hiyo imewezesha wananchi katika maeneo mengi ya vijijini kupata huduma za simu na internet kwa mara ya kwanza au kwa ubora zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Kwa mwanafunzi, mnara unaweza kuwa njia ya kupata taarifa za masomo.

Kwa mkulima, unaweza kuwa njia ya kupata bei za mazao.

Kwa mfanyabiashara, unaweza kuwa njia ya kufikia wateja wapya.

Kwa lugha rahisi, kabla ya uchumi wa kidijitali kulikuwa na mawasiliano. Na kabla ya mawasiliano kulikuwa na miundombinu.

Kilomita 13,820 Zenye Thamani Kubwa

Kama barabara zinavyobeba magari na reli kubeba mizigo, uchumi wa kidijitali nao una miundombinu yake.

Miundombinu hiyo ni Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Katika miaka ya karibuni, Serikali kupitia TTCL imeendelea kupanua Mkongo wa Taifa hadi kufikia zaidi ya kilomita 13,820 huku wilaya zaidi ya 120 nchini zikiunganishwa.

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amekuwa akisisitiza kuwa Mkongo wa Taifa ni uti wa mgongo wa uchumi wa kidijitali kwa kuwa unawezesha taasisi za umma, sekta binafsi, shule, hospitali na wananchi kupata huduma za mawasiliano kwa uhakika zaidi.

Kadiri miundombinu hiyo inavyopanuka, ndivyo gharama za mawasiliano zinavyopungua na fursa za biashara na uwekezaji zinavyoongezeka.

Kwa wataalamu wa teknolojia, Mkongo wa Taifa ni sawa na barabara kuu ya uchumi wa kidijitali wa Tanzania.

Bila mkongo huo, huduma nyingi za internet, biashara za mtandaoni na mifumo ya kidijitali isingeweza kufanya kazi kwa kiwango kinachoonekana leo.

Internet Kama Chanzo cha Kipato

Mabadiliko hayo ndiyo yanayoonekana kwa vijana kama Baraka Mafole.

Kupitia kazi za mtandaoni, amegeuza ujuzi wa lugha kuwa chanzo cha kipato kinachovuka mipaka ya Tanzania.

Hadithi kama hizi zinaanza kuongezeka kadiri internet inavyopatikana kwa wananchi wengi zaidi.

Leo vijana wengi wanapata kazi kupitia majukwaa ya kidijitali katika maeneo kama tafsiri, uandishi wa maudhui, masoko ya kidijitali, usanifu wa picha, programu za kompyuta na huduma mbalimbali zinazouzwa katika soko la kimataifa.

Kwa wachumi, hii ni hatua muhimu kwa sababu huduma hizo huingiza fedha za kigeni nchini bila kuhitaji usafirishaji wa bidhaa.

Katika ulimwengu wa kidijitali, maarifa na ujuzi vinaweza kuwa bidhaa.

Mitandao ya Kijamii Kama Soko

Wakati baadhi ya watu wakitumia mitandao ya kijamii kwa burudani, Ibrahim Chenza aliiona kama fursa ya biashara.

Kupitia Facebook, Instagram, YouTube na majukwaa mengine ya kidijitali, ameweza kufikia maelfu ya watu ambao asingewaona kupitia njia za kawaida za biashara.

Leo, sehemu ya ukuaji wa biashara zake imejengwa juu ya uwezo wa kufikia wateja kupitia internet.

Kwa wataalamu wa biashara, huu ni mfano wa namna teknolojia inavyobadilisha dhana ya soko.

Badala ya kutegemea eneo moja la biashara, mfanyabiashara anaweza kufikia wateja katika mikoa yote ya Tanzania na hata nje ya nchi kwa kutumia simu janja na internet.

Hii ndiyo sababu sekta ya TEHAMA imeanza kuonekana kama sehemu muhimu ya uchumi, si sekta ya mawasiliano pekee.

Miundombinu Inapozaa Ubunifu

Lakini uchumi wa kidijitali hauishii kwenye biashara za mtandaoni.

George Machibya, mmoja wa wadau wa sekta ya teknolojia, anaona mabadiliko makubwa katika mazingira ya ubunifu nchini.

Anasema maendeleo ya internet, mifumo ya malipo ya kidijitali na majukwaa ya kiteknolojia yamefungua fursa mpya kwa vijana wanaotaka kuanzisha biashara za kidijitali.

Miaka kadhaa iliyopita, ilikuwa vigumu kwa startup nyingi kupata mazingira ya kukua.

Leo, vijana wanaweza kujenga huduma za kidijitali zinazotumiwa na maelfu ya watu ndani na nje ya Tanzania.

Hii imechangia kuibuka kwa biashara mpya katika maeneo ya fintech, e-commerce, digital marketing, software development na huduma nyingine za kidijitali.

Kwa lugha rahisi, Mkongo wa Taifa haujasafirisha data pekee.

Umesafirisha pia mawazo, ubunifu na biashara mpya.

Zaidi ya Watumiaji, Tanzania Inahitaji Wabunifu

Hata hivyo, viongozi wa sekta ya mawasiliano wanaamini kuwa mafanikio ya kweli hayatapimwa kwa idadi ya watumiaji wa internet pekee.

Yatapimwa kwa idadi ya wabunifu, watengenezaji wa teknolojia na wajasiriamali watakaoibuka kutokana na uwekezaji huo.

Ndiyo maana TCRA imeendelea kuhamasisha uanzishwaji wa vilabu vya kidijitali kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu.

Akiwasilisha mada katika mkutano wa TAPSHA, Meneja wa Masuala ya Wateja na Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano wa TCRA, Mhandisi Kadaya Baluhye, alisema lengo ni kuwahamasisha vijana kupenda masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) na kuwajengea msingi wa matumizi yenye tija ya TEHAMA.

Kwa mujibu wa TCRA, vilabu hivyo vinakusudia kuwakutanisha vijana katika majukwaa ya kujifunza, kufanya majaribio ya teknolojia na kukuza ubunifu ambao unaweza kuzaa biashara na ajira za baadaye.

Hii ni sehemu ya mkakati wa kuandaa kizazi kitakachoshiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali badala ya kuwa watumiaji wa teknolojia pekee.

Safari Bado Inaendelea

Pamoja na mafanikio hayo, wataalamu wanaona kuwa Tanzania bado ina kazi kubwa mbele yake.

Changamoto si tena kupeleka internet kwa wananchi pekee.

Changamoto ni kuhakikisha internet inatumika kuzalisha thamani ya kiuchumi.

Kwa sasa sehemu kubwa ya matumizi ya internet bado inaelekezwa katika mawasiliano, burudani na matumizi ya kawaida ya mitandao ya kijamii.

Hatua inayofuata ni kuongeza matumizi ya teknolojia katika biashara, elimu, kilimo, afya, ubunifu, utafiti na uzalishaji wa maudhui.

Hapo ndipo Taifa litaweza kuvuna kikamilifu matunda ya uwekezaji mkubwa uliofanywa katika miundombinu ya kidijitali.

Kutoka Mawasiliano Hadi Uchumi

Miaka michache iliyopita, internet ilikuwa anasa kwa sehemu kubwa ya Watanzania.

Leo imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

Lakini thamani yake kubwa zaidi inaweza isiwe kwenye ujumbe unaotumwa au video zinazotazamwa.

Inaweza kuwa kwenye biashara zinazozaliwa, ajira zinazopatikana, huduma zinazobuniwa na mapato yanayozalishwa.

Kutoka kwa kijana anayepata kipato kupitia Kiswahili mtandaoni hadi wanafunzi wanaojiandaa kuwa wabunifu wa kesho kupitia vilabu vya kidijitali, ushahidi unaanza kuonesha kuwa mapinduzi ya kidijitali ambayo Serikali ilianza kuyajenga miaka michache iliyopita yanaanza kuonekana katika maisha ya wananchi.

Swali lililobaki si kama Tanzania imeingia kwenye uchumi wa kidijitali.

Swali ni jinsi gani Watanzania wengi zaidi wataweza kushiriki, kunufaika na kuujenga uchumi huo katika miaka ijayo.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button