Tanzania yang’ara miradi ya Kinywe

RIPOTI ya Benki ya Dunia na Takwimu za Taasisi ya Jiolojia ya Marekani kuhusu makisio ya utajiri wa mashapo ya Madini ya Kinywe ifikapo mwaka 2050 imeitaja nchi ya Tanzania kushika nafasi ya Sita (6) Duniani na nafasi ya Tatu (3) Afrika huku Msumbiji ikishika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Madagascar kwa upande wa nchi za Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dk Venance amesema hayo wakati akimwakilisha Waziri wa Madini, Anthony Mavunde katika mjadala wa Mawaziri uliofanyika katika Kilele cha Mkutano wa Madini Muhimu Afrika, Cape Town, Afrika Kusini na kwamba, Tanzania imebarikiwa kuwa na aina nyingi za madini muhimu yanayohitajika kwa ajili ya uzalishaji wa nishati na teknolojia za kisasa.

Amesema Tanzania imejipanga katika ugunduzi wa madini ya kinywe na madini mengine ya nishati safi kama nikeli, Cobalt, lithium, rare earth elements na nobium kwa kuwa na taarifa za kutosha za kijilojia.
SOMA: Wizara ya Madini waja kisasa zaidi
“Tanzania imeanza kutekeleza Madini Vision2030 yenye lengo la kupunguza uwezekano wa wawekezaji kupata hasara kwa kufanya tafiti maeneo ambayo hayana taarifa za kijilojia ‘derisking the sector”, amesema.

Lengo la mkakati huo ni kufanya utafutaji wa madini kwa njia ya ndege (High Resolution Airbone Survey) kutoka asilimia 16 ya sasa na kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.
Dk Mwasse ameeleza kuwa ni muhimu sasa kwa nchi za Afrika kuwa na ushirikiano wa kuongeza thamani madini muhimu kwa kuweka viwanda katika nchi ambayo itakuwa inafaa kwa nchi nyingine za afrika.

“Ni wakati mwafaka wa nchi za Afrika kufanya uchambuzi wa faida na hasara ‘cost benefit analysis” kuona sehemu sahihi ya kuweka mitambo ya kusafisha na kuongeza thamani madini muhimu” ameongeza mfano kiwanda kitakachojengwa cha Kabanga Nickel multi-metal smelter cha Kahama kitawezesha nchi jirani kama Burundi na Congo.



