TANZANIA inazidi kupata mafanikio kwenye sekta ya fedha, imefahamika.
Kwa mujibu wa ripoti ya viashiria vya Masoko ya Fedha ya Absa (AFMI) ya mwaka 2024, Tanzania imepanda kutoka alama 50 hadi 52.
Kutokana na mafanikio hayo, imeshika nafasi ya 12 miongoni mwa mataifa 29 yaliyotathminiwa Afrika.
AFMI ni ripoti ya matokeo ya kupima maendeleo ya sekta ya fedha katika nchi za Afrika, ikitathmini vigezo sita.
Vigezo hivyo ni pamoja na kuenea kwa soko, upatikanaji wa fedha za kigeni, uwazi kwenye soko na kanuni, maendeleo ya mifuko ya pensheni, mazingira ya uchumi ngazi ya kitaifa na kutekelezeka kwa makubaliano ya kifedha.
Wakati wa uzinduzi wa ripoti ya AFMI 2024 Dar es Salaam, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel
Tutuba alipongeza Absa Group kwa kujitolea kukuza uwazi na ufanisi katika masoko ya fedha barani kupitia ripoti ya AFMI.
“Mafanikio yaliyobainishwa katika ripoti hii ni ushahidi wa juhudi za ushirika miongoni mwa serikali, Benki Kuu
ya Tanzania na washirika wa soko la fedha katika kuboresha masoko hayo,” alisema Tutuba.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, miongoni mwa maeneo ambayo Tanzania imeonesha kupiga hatua ni upatikanaji wa fedha za kigeni ikipanda kutoka alama 53 hadi alama 60.
Mafanikio hayo yamechangiwa na BoT kuchapisha miiko ya utendaji katika soko la fedha za kigeni miongoni mwa benki ikiingiza kanuni 52 kati ya 55 zinazotambuliwa kimataifa.
Eneo la pili lililoipandisha Tanzania ni uwazi katika mazingira ya uchumi ngazi ya kitaifa.
Katika hilo, Tanzania imepanda kutoka alama 80 hadi 85 ikichagizwa na uwazi, ikiwemo umma kuruhusiwa kufahamu ratiba ya mkutano wa sera ya fedha, mfumuko mdogo wa bei na kupungua kwa uwiano wa mikopo chefuchefu kwenye kampuni ya biashara.
Eneo la tatu ni uwezo wa soko la fedha kufikia watu wengi zaidi na maendeleo katika hilo yanatokana na kutolewa
kwa dhamana za kampuni zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 300 na kuzinduliwa kwa huduma za kifedha, ikiwemo zinazorandana na maadili ya dini ya Kiislamu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser alisisitiza umuhimu wa ripoti ya AFMI katika kuchochea kukua kwa masoko ya fedha Afrika.