Tanzania yanufaika na GPE
yatia kibindoni Dola za Marekani mil. 207, Dola mil.50 mbioni kutua
TAASISI ya Ushirikiano wa Elimu Dunia ((GPE) imeipatia Tanzania Dola za Marekani milioni 207.3 kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini.
Fedha hizo zimetolewa kwa awamu mbili mwaka 2014/2018 na 2019 mpaka 2025.
Hayo yamesemwa leo Agosti 31, 2023 na Mwenyekiti wa Bodi ya GPE, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete katika hafla ya uchangiaji wa fedha za maboresho ya elimu nchini.
Kikwete amesema fedha hizo zimeelekezwa kwenye ujenzi wa madarasa, vyoo, nyumba za walimu na vifaa vya shule.
Aidha, amesema mwaka huu GPE itatoa Dola za Marekani milioni 50 ikiwa ni mwendelezo wa kuboresha sekta ya elimu ya Awali, Msingi na Sekondari
“Nchi yetu ya Tanzania ni mshirika GPE tangu mwaka 2013 mpaka sasa GPE imechangia Dola za Kimareni milioni 207.3 sawa na bilioni 500 na ushee na zimeelekezwa elimu ya awali na msingi.”Amesema Kikwete
Amesema, awamu hizo mbili mchango wa GPE umeweza kujenga madarasa zaidi ya 2000
Aidha, Kikwete amesema GPE itachangia Dola moja kwa kila shilingi moja itakayochangiwa.
“watoto wa mjini wanasema kutoa cha juu, GPE inatoa cha juu kwa kila dola moja ya Marekani itakayopatikana kupitia ufadhili wa sekta binafsi kama vile Kampuni, Asasi za Kiraia au Mabenki, Taasisi ya GPE nayo itatoa Dola moja ya Marekani kwa kila shilingi moja .
“Mkichangia nyingi, GPE inatoa nyingi, mkichangia kidogo GPE itatoa kidogo, lakini pia kwa kila Dola 3 za Marekani zitakazotolewa kama msaada au msamaha wa Kodi, kutoka taasisi za fedha za Kimataifa, au nchi Washirika wa Maendeleo, Taasisi ya GPE nayo inatoa Dola moja.”Amesema Kikwete na kuongeza
“Pia kama nchi inamikopo IMF nchi ikifanikiwa kuongea na anayewadai kwa kila Dola 3 inayosamehewa, GPE inachangia Dola 3 kwa masharti ya fedha zinazosamehewa kuingizwa kwenye sekta ya elimu.
“Mfano, mnafanya mazungumzo na Uingereza bwana tusamehe deni hili, hizo fedha ambazo tungekulipa wewe hizo pesa tutazitumia Kwa ajili ya elimu.
“Uingereza iseme tunawasamehe Dola 10,000 Kwa masharti kwamba muelekeze kwenye elimu, ukishapata huo msamaha GPE kwa kila Dola 3 inachangia wao. ” Amesema Kikwete na kufafanua zaidi
” Utaratibu huu wa kibunifu unalenga kupatikana fedha kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu na kuongeza uwekezaji, kutoa fursa kwa wadau kushirikiana kwa pamoja kuendeleza sekta ya elimu.” Amesema
Amesema GPE ni Shirika lililoanzishwa miaka 20 iliyopita na mataifa saba makubwa duniani sio Shirika jipya shabaha yake ni kusaidia elimu katika nchi za kipato cha chini na hadi sasa inasaidia nchi 88.