Tanzania yaongoza kwa nyati wengi Afrika

TANZANIA inatajwa kuwa nchi inayongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya nyati barani Afrika kwa kuwa na jumla ya nyati 191,805.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana leo Novemba mosi, 2022 jijini Arusha, wakati akitangaza matokeo ya sensa ya wanyamapori iliyofanyika mwaka huu.

Waziri Chana amesema nyati hao wengi wanapatikana katika mifumo ikolojia ya Serengeti (69,075) Nyerere-Selous-Mikumi (66,546), Katavi-Rukwa (35,273) pamoja na   Ruaha-Rungwa ( 20,911).

Lengo kuu la Sensa hiyo, ambayo hufanyika kila baada ya miaka mitatu katika mfumo Ikolojia ya Katavi –Rukwa na Ruaha-Rungwa ni kujua uwepo, idadi, mtawanyiko pamoja na viashiria hatarishi kwa ustawi wa wanyamapori nchini Tanzania.

Pia Dkt Chana amesema idadi ya Wanyama hao imeendelea kuongezeka hasa katika maeneo ya ndani ya hifadhi, ambapo nyati hao wameongezeko kwa asilimia 64 kutoka mwaka 2018.

“licha ya kuwepo kwa changamoto za mifugo katika mifumo ya ikolojia, nyati wameongezeka na hii ni kiashiria kizuri cha udhibiti wa mifugo kwenye maeneo yaliohifadhiwa,” alisema Waziri huyo

Akizungumzia matokeo ya sensa katika mfumo wa ikolojia wa Katavi Rukwa, Waziri Chana amesema idadi ya tembo imeendelea kuimarika na viashiria vya ujangili wa tembo vimeendelea kupungua ukilinganisha na sensa ya mwaka 2018.

Alifafanua kuwa mwaka 2021, uwiano wa mizoga mipya ya tembo ilikuwa asilimia 3 wakati mwaka 2018 ilikuwa asilimia 12.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema kuwa katika mfumo wa Ikolojia wa Ruaha- Rungwa idadi ya wanyamapori adimu kama korongo na palahala, imeendelea kuongezekam, ambapo Korongo wameongezeka mara mbili kutoka korongo 1,436 mwaka 2018 hadi 3,127 kwa sensa ya mwaka 2021.

 

Habari Zifananazo

Back to top button