Tanzania yapongezwa kupinga ukatili wa kijinsia

Dar es Salaam : UMOJA wa Mataifa umeipongeza serikali ya Tanzania kwa kuwa kinara wa kupinga ukatili wa kijinsia kwa vitendo kwa kuzingatia usalama wa jinsia kuanzia ngazi ya Polisi Kata hadi Taifa jambo ambalo ni la kuigwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 16,2023 Chuo Kikuu cha Dar es Salaaam (UDSM), wakati wa mdahalo wa kujadili malengo endelevu ya dunia ambayo yamewakusanya wadau na zaidi ya wanafunzi 300 kutoka vyuo na shule za sekondari, Mratibu Mkaazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Zlatan Milisic amesema Tanzania inafaa kuigwa kwa kusimamia malengo ya dunia.

Amesema moja ya mambo muhimu ni kuzingatia usawa wa haki za wengine na kuwa mstari wa mbele katika kupinga ukatili wa kijinsia kwa kuweka usimamizi wa madawati ya jinsia kila kituo cha polisi.

Advertisement

Kwa upande wake, Ofisa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Mratibu Wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Nafsa Didi amesema Tanzania ni nchi mojawapo ambazo zimevuka malengo hayo ambapo yamewasilishwa jijini New York, Marekani lengo likiwa ni kuhamasisha vijana kuwa mstari wa mbele katika kupinga uchafuzi wa mazingira na kukataa ukatili miongoni mwa jamii.

Miongoni mwa washiriki wa mdahalo huo ni Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Hamis Seif na baadhi ya wanafunzi kutoka vyuo na shule mbalimbali za sekondari, Martina Makarios na Derick Jacob, wameipongeza serikali kuwa sehemu muhimu ya kutambua thamani ya usawa wa kijinsia na kuwaamini vijana kuwa mabalozi wazuri wa utunzaji wa mabadiliko ya tabianchi kwa kuikomboa jamii.

Mdahalo huo ni maandalizi ya mkutano mkubwa unaotarajiwa kufanyika nchini Marekani Septemba 18 hadi 19 mwaka huu, ambapo moja ya ajenda ni kujadili malengo endelevu ya dunia namna gani yamefikiwa katika nyanja mbalimbali.

6 comments

Comments are closed.

/* */