Tanzania yatafuta fursa za ajira Qatar

UJUMBE wa Serikali ya Tanzania umejadiliana na uongozi wa Hamad Medical Corporation (HMC) jijini Doha, Qatar kuhusu namna ya kuanza kutoa nafasi za ajira kwa Watanzania katika sekta ya afya.

Ujumbe wa serikali uliongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Profesa Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab.

Wataalamu wa sekta ya afya nchini Tanzania walikuwa hawajaanza kuingia kwenye soko la ajira la Qatar na hivyo endapo Tanzania itafunguliwa nafasi hizo, itapeleka wataalamu kufanya kazi nchini humo.

Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi, Idara ya Rasilimali Watu wa ‘Hamad Medical Center’, Sabeeha Amin Qasemi amesema hospitali hiyo imefurahishwa na hatua ambazo Tanzania inazichukua kuboresha sekta ya afya na kuahidi kuwa watatoa nafasi za ajira kwa wataalamu wa afya ambao hatimaye watapelekwa kwenye hospitali Qatar.

Profesa Katundu aliueleza uongozi wa shirika hilo kuwa Tanzania ina wataalamu wa afya wenye uwezo na uzoefu na endapo watapata fursa za ajira huko, watafanya kazi kwa bidii na weledi kwa kuzingatia sheria na taratibu za Qatar.

Balozi Fatma alisema Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Qatar ili kuiwezesha kupata wafanyakazi bora zaidi katika sekta mbalimbali.

Awali, ujumbe wa Tanzania na Qatar walijadiliana namna bora ya kuendelea kutekeleza mkataba wa ajira uliosainiwa kati ya Tanzania na Qatar mwaka 2014.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi Qatar, Mohammed Hassan Al-Obaidly alisema Serikali ya Qatar imeanza mchakato wa kuanzisha kituo maalumu cha viza nchini Tanzania ili kurahisisha namna ya kupata Watanzania watakaokwenda kufanya kazi Qatar.

Ikiwa kituo hicho kitaanzishwa Tanzania, kitakuwa cha kwanza kujengwa barani Afrika, vingine vikiwa India na Ufilipino, nchi ambazo zinatoa idadi ya wafanyakazi kwenda kufanya kazi Qatar.

Al-Obaidly aliahidi kuwa Serikali ya Qatar itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kupata Watanzania wenye sifa za kuajiriwa humo kwa kutumia mifumo yao ya ajira.

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button