TARI kutumia chupa kuzalisha mbegu

ILI kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI), imeweka mikakati katika utafiti wanaoufanya kwa kuwa na mbegu ambazo zinakinzana na magonjwa, ukame na zinazaa kwa wingi.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kushirikiana na halmashauri mbalimbali nchini na wadau katika kugawa mbegu ambazo zimefanyiwa utafiti kwenye mikoa ambayo inalima nazi nchini, ili waweze kustawisha vitalu vyao katika zao la minazi.

Mratibu wa Uhaulishaji Teknolojia na Uhusiano Kituo cha TARI Mikocheni, Dar es Salaam, Vidah Mahava  amesema kumekuwa na changamoto kwa jamii kutojua kuhusiana na kituo hicho, lakini  na uzalishaji wa mbegu kwa njia ya chupa.

“Watu wengi wanakuwa na taarifa tofauti, wengine wanafikiria kwamba tukienda Mikocheni kuwa ni GMO wanaiweka bioteknolojia na GMO kumbe yote hayo yanatokana na wananchi kutokuwa na taarifa kamili kuhusiana na kituo hiki na utafiti wetu unavyofanya kazi,” amesema Vidah.

Amesema hicho ndicho kituo pekee kinachosimamia zao la minazi na malengo yao ni kuhakikisha kuwa linachangia pato la taifa na mazao ya mafuta.

Ameeleza kuwa kwa sasa nazi wanazozigawa zina uwezo wa kuzaa nazi 35 mpaka 45, ambapo utafiti unataka kufika mpaka nazi 70, hivyo kuna mbegu ambazo wamekuwa wakizigawa kwa wadau wao.

“Mikakati mikubwa ambayo tunaifanya ni kuhakikisha tunaweza kufanya kazi na wadau mbalimbali, ili kufufua zao la minazi kwa kutumia kanuni bora za kilimo.

Mahava amesema  kuwa TARI inafanya utafiti wa mazao kwa kuvumbua mbegu kwa kutatua matatizo ya wakulima nchini, ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mazao yao hususani wadudu.

Naye Mtafiti Kituo cha TARI Mikocheni kwa upande wa maabara ya Tissue Culture, Christina Kidulile amesema katika maabara hiyo wanazalisha mimea ya aina mbalimbali ukiwemo mkonge,viazi vitamu na wamekuwa wakitumia vifaa mbalimbali vinavyosaidia mimea kuota.

Habari Zifananazo

Back to top button