Tarura wapewa wiki majibu ujenzi wa barabara

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga limetoa wiki moja kwa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini(TARURA ) kuhakikisha wanatoa majibu juu ya hatua waliyochukuwa kuhusu ujenzi wa barabara ya kwenda Dampo Kata ya Kizumbi kutokana na miundombinu yake kuharibika.

Agizo hilo limetolewa na Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko kwenye kikao cha Baraza la Madiwani ambapo amesema barabara hiyo ina changamoto kubwa na imekuwa ikitolewa maelezo bila utekelezaji.

Amesema halmashauri hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika suala la usafi wa mazingira kutokana na kuwa na utaratatibu mzuri wa kuzoa taka zinazozalishwa kwenye mitaa mbalimbali hivyo ni muhimu barabara hiyo kutengenezwa kabla miundombinu yake haijaharibika zaidi.

Advertisement

“Ili kuepuka kutokea athari kubwa ninatoa wiki moja niwe nimepata majibu kutoka Tarura juu ya barabara hii ,kwani ni muhimu sana kutokana na halmashauri yetu kufanya vizuri kwenye suala la usafi hivyo ni muhimu kutengenezwa kabla ya mvua za masika kuzidi,”amesema Mstahiki Meya Masumbuko.

Awali Diwani wa Kata ya Kizumbi, Reuben Kitinya alitaka kujua mpango uliopo wa kuboresha miundombinu ya barabara ya dampo kipindi hiki kutokana na kuwa na changamoto kubwa ya miundombinu yake kuharibika .

Akitoa ufafanuzi Kaimu Meneja wa Tarura Wilaya  ya Shinyanga,  Mhandisi Kulwa Maige amesema barabara hiyo haikuwekwa kwenye bajeti na kuahidi kulifanyia kazi agizo lililotolewa ili kutatua changamoto hiyo.