Tarura yafanya kweli barabara Misenyi

KAGERA; WAKALA wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera amekamilisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami eneo la Bunazi, Kata Kasambya.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo, Meneja wa Tarura Wilaya ya Missenyi, Mhandisi Ally Maziku amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutawezesha wananchi kupita kwa urahisi.
“Kutengenezwa kwa barabara hii kwa kiwango cha lami imewezesha wananchi kupita kiurahisi na kuleta faida kama kukua kwa shughuli za kiuchumi na kuondoa matengenezo ya mara kwa mara,” amesema Maziku.
Amesema kuwa kati ya kilomita tano zilizokusudiwa kutengenezwa kwenye Wilaya ya Missenyi, kilomita tatu zimeshakamilika na kwa matengenezo mradi wa njia nne, zikiwa mbili kwenda na mbili kurudi umefikia asilimia 95 na sasa upo kwenye kipindi cha matazamio.
Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Florance Kyombo ameishukuru serikali kwa kuongeza kiwango cha bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, kwani imesaidia kutatua changamoto za wananchi wakati wa kusafiri na kusafirisha bidhaa zao.
Soma pia: Mradi wa maji Misenyi wafikia asilimia 90
“Ndani ya Wilaya ya Missenyi kipindi cha nyuma bajeti ya barabara ilikuwa ni Sh milioni 700 tu, lakini hivi sasa tunapata Sh bilioni 2.4 kwa mwaka,” amesema Kyombo.
Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Godfrey Mnzava ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kuweka jiwe la msingi na kuipongeza Tarura, Wilaya ya Missenyi kupitishwa mfumo wa manunuzi kidigitali.
“Mwenge wa Uhuru umeridhika kuwa kazi imefanyika vizuri na mwenge wa Uhuru utaweka jiwe la msingi katika mradi huu wa ujenzi wa barabara na niwapongeze Tarura kuzingatia mfumo wa manunuzi wa kidijitali,” amesema Mnzava



