TASAC yaboresha kanuni kuongeza ufanisi

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),  limesikia kilio cha wadau wa sekta ya usafiri kwa njia ya maji kwa kuboresha kanuni mbalimbali ambazo zimekuwa ni kikwazo katika utendaji wao wa kila siku.

Akizungumza kwa niaba ya wadau hao wa sekta ya usafiri kwa njia ya maji, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Edward Urio amesema maboresho yaliyofanyika yamegusa maeneo yaliyokuwa na utata mwingi katika utendaji wao.

Amesema upande wa mawakala wa forodha walikuwa na utata katika ule muda wa kontena linaposhuka bandarini na linapofika kwenye bandari kavu, ambako kulikuwa na upotevu wa siku mbili au tatu kwa kuhoji jambo hilo lilipaswa kubebwa na nani jambo ambalo kanuni hizo zimekuja na majibu yake.

“Lakini kuna suala moja kubwa kama unaagiza mzigo kwa kupitia bandari hasa mzigo wa makasha, kuna utaratibu ambao unatakiwa uweke dhamana ya kuweza kuaminiwa na wale mawakala wa meli uweze kulichukua lile kisha ukapakue mzigo wako.

“Kama ni hapa Dar es Salaam, kama ni Morogoro, kama ni Arusha, kama ni Malawi, Zambia, Congo, halafu ile dhamana ya lile kontena inakuwa iko chini kwa wakala wa forodha mpaka litakapokuwa limerudi kwenye sehemu yake husika ya kurudisha,” amesema.

Kwa maelezo yake gharama hiyo ilikuwa ni kubwa ambapo asilimia kubwa ya wanachama wao ambao ni Watanzania walikuwa hawawezi kuzimudu.

“Tulikuwa tunatakiwa kuweka takribani dola 3000 mpaka 5000 kwenye makasha ya futi 40 na dola 1000 mpaka 2000 kwenye makasha ya futi 20. Unakuta kuwa ukiwa na kontena 10 ya futi 40 unatakiwa ulipe takriban dola  40,000,” amesema.

Amesema dola hizo 40,000 kwa wakala ambaye analipwa dola 200 kwa kila kontena ilikuwa ni maumivu makubwa.

Naye Mkurugenzi wa Udhibiti Huduma za Usafiri kwa njia ya maji TASAC, Deogratias Mukasa amesema wamekutana na wadau wao kutoa ufafanuzi kuhusu kanuni mpya nne ambazo zimepitishwa Juni mwaka huu.

Amesema kanuni hizo zinahusu usalama wa mizigo, utendaji wa shughuli ndani ya bandari na bandari kavu, usajli wa wasafirishaji wanaouza na kusafirisha bidhaa kutoka Tanzania kwenda nchi za nje kupitia bandari, pamoja na ya uhakiki shehena na ya uwakala wa meli.

Amewataja wadau waliokutana nao ni bandari, bandari kavu, mawakala wa meli, wagomboaji wa shehena, wakusanyaji na watawanyaji shehena, wasafirishaji na mamlaka ya forodha.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Kaimu Mkeyenge amesema shirika hilo linathamini utoaji elimu kabla ya kuanza utekelezaji wa sheria au kanuni zake, na kwamba maboreesho ya kanuni hizo yanalenga kuboresha utoaji huduma kwa usahihi na kuleta usawa kwa wadau wote.

 

Habari Zifananazo

7 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button