MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kuanzia mwezi Julai 2021 hadi Juni 2024 mpango imehawilisha ruzuku ya jumla ya Sh bilioni 945.5 kwa kaya milioni 1.37 zilizoandikishwa kwenye mpango huo huku kaya za walengwa 534,606 zikilipwa kwa njia ya kielektroniki.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mifumo kutoka makao makuu, Japhet Boazi akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Tasaf, Shadrack Mzirai amesema hayo leo katika kikao cha kujengeana uelewa kwa viongozi na waandishi wa habari mkoani Shinyanga.
Boazi amesema kipindi cha mpango wa pili ambacho kilizinduliwa mwezi Februari ,2020 kimeendelea kuhudumia zaidi ya kaya milioni 1.37 na utekelezaji wake inafanyika kwenye halmashauri 184 Tanzania Bara na upande wa Zanzibar kwa Unguja na Pemba.
Boazi amesema katika mpango wa utoaji ajira za muda miradi 27,863 iliibuliwa na wananchi na kutekelezwa na walengwa wa mpango ambapo kiasi cha Sh bilioni 117.3 kimetumika kulipa ujira kwa kaya za walengwa 662,374 kwa kushiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Tasaf ilianza kutekelewa kipindi cha kwanza cha mpango wa kunusuru kaya maskini mwaka 2013 baada ya kuzinduliwa mwaka 2012 ikilenga kuhudumia kaya milioni 1.2 ambazo zilikuwa chini ya mstari wa umasikini wa chakula,”amesema Boazi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Annamringi Macha akifungua kikao hicho amesema Tasaf imeweza kuondoa umasikini kwenye kaya zilizokuwa zimelengwa nakufikia hatua ya kuondoka kwenye mpango wa kujinusuru na umaskini kwa kufuga mifugo,kujengwa nyumba zilizoezekwa kwa bati badala ya nyasi.
“Wapo baadhi ya watu wamekuwa wakibeza mpango huo kuwa wanafanyishwa kazi kama wafungwa kwa kweli kama huelewi vizuri utaratibu utasema lakini ukiuelewa hutasema kwa kubeza vyombo vya habari viendelee kuelimisha zaidi,”amesema Macha.