CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), kuanzia Julai mwaka huu kitaanza kutoa Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Tanzania wa kila mwezi.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu wa TASWA, Alfred Lucas imeeleza kuwa tuzo hiyo ilikuwa ikitolewa miaka ya nyuma na chama hicho, lakini miaka ya karibuni haikuwa ikitolewa, hivyo kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kilichofanyika Aprili 30,2023 kilifikia uamuzi wa kuirejesha tena tuzo hiyo.
“Tuzo hiyo itakayoanza kushindaniwa mwezi Julai, 2023 na mshindi wake kupatikana Agosti 2023, itahusisha wanamichezo wote wanaocheza Tanzania, ambao michezo yao inatambuliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na wale ambao ni Watanzania lakini wanacheza nje ya Tanzania.
“Baada ya kupatikana mshindi wa kila mwezi kwa mwaka mzima 2023/2024, TASWA itaandaa sherehe za Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Tanzania kwa mwaka, ambaye mshindi wa jumla atatoka miongoni mwa washindi wa mwezi.
“Pia katika sherehe hizo TASWA itazawadia wanamichezo wengine waliofanya vizuri kwa michezo yote inayotambuliwa na BMT, ambao kwa mwaka 2023/2024 michezo yao itakuwa imefanya mashindano kitaifa au kimataifa na kuonekana wanastahili tuzo.
“Jukumu la uratibu wa tuzo hiyo ya kila mwezi pamoja na ile ya mwaka litasimamiwa na Kamati ya Tuzo za TASWA, ambayo tayari imeundwa na itatangazwa hivi karibuni,” amesema Lucas.