Tatu apotea mazingira ya kutatanisha Sirari

GEITA: TATU Paulo (46) mkazi wa mtaa wa Stamico, mamlaka ya mji mdogo wa Katoro wilayani Geita ameripotiwa kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha akiwa wilayani Sirari hali iliyoibua taharuki kwenye familia yake.
Mume wake Tatu, ambaye ni mfanyabiashara wa pembejeo za kilimo na mifugo katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro, Yohana Zacharia alisema mke wake aliondoka nyumbani tangu Machi 02, 2025.
Yohana amesema hayo mbele ya waandishi wa habari na kueleza, awali mkewe aliondoka nyumbani machi 02, 2025 kuelekea Nzega akiambatana na kijana mmoja ambaye alikuwa anamsindikiza kwa shughuli za uchumba.
Amesema mke wake na kijana huyo walitumia usafiri binafsi (gari ya familia) na walitoa taarifa kuwa majira ya jioni ya siku hiyo waliwasili salama Nzega bila tatizo lolote.
Amesema siku ya Machi 03, 2025 majira ya saa moja usiku alipigiwa simu na mkewe kumuarifu amerejea Katoro lakini hatofika nyumbani kwa sababu anaelekea Silari amepata taarifa mzigo wake umekamatwa.
“Majira ya saa tatu asubuhi, (Machi 04, 2025) akanipigia simu kwamba mimi nimeshafika Silari, mchana sikumtafuta tena ilipofika jioni wakati nafunga biashara nikampigia simu kumuuliza mzigo umefikia wapi.
“Nilipoanza kupiga simu ikawa haipatikani, niliporudi nyumbani nikawauliza mbona huyu simu yake haipatikani labda nyie ameshawapigia, wakasema hapana”, ameeleza.

Yohana amesema alifanya juhudi za kuwasiliana na ndugu na watu wa karibu na mkewe lakini wote walikana kuwa hawajamuona Tatu na wala hawajawasiliana naye.
Amesema alisafiri kuelekea Silari na kwenda mpaka kituo cha polisi kuulizia iwapo mke wake anashikiliwa ama kuna mzigo wa bidhaa za pembejeo za kilimo na mifugo umekamatwa lakini polisi walikana.
“Ikabidi twende TRA, tukauliza, nao wakasem hatujaona mtu kama huyo, na wala hatujakamata mzigo wowote hapa, tukavuka kwenda Kenya, kituo cha polisi mpakani nao wakasema hawana taarifa.
“Tukaenda uhamiaji, nao tukawauliza wakasema hawatambui kitu chochote, TRA hawajui kitu chochote, ikabidi nirudi nitoe taarifa kwa RCO (Ofisa Upelelezi Mkoa), ndio akaniomba namba ili ashughulikie”, amesimulia.
Kaka yake Tatu, Chacha William amesema hofu yao kubwa ni kwamba inawezekana ndugu yao ametekwa, au ametendewa jambo baya na kuiomba serikali kupitia jeshi la polisi liwasaidie kumpata ndugu yao.
Habarileo imefanya mawasiliano kwa njia ya simu na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rolya, Mark Njera ambaye alijibu kupitia ujumbe mfupi wa simu kuwa bado hana taarifa ya tukio hilo mpaka sasa.



