Tausi Likokola kurudi tena kwa jamii

Mwanamitindo mstaafu wa kimataifa, Tausi Likokola.

MWANAMITINDO mstaafu wa kimataifa, Tausi Likokola amesema anaandaa ‘documentary’ ambayo sehemu ya mapato yake atarudisha kwa jamii.

Likokola amesema kipindi cha nyuma alianza kupeleka kahawa ya Tanzania nchini Marekani na kupitia hilo alisaidia baadhi ya wakulima hata hivyo amesema ataendelea kusaidia kwa atakavyoweza.

Akizungumza na HabariLEO, Likokola amesema katika kuendelea na jitihada za kusaidia jamii wakiwemo wasichana, anapanga kuirudisha taasisi yake nchini.

Advertisement

SOMA: Wanamitindo wa kimataifa watakiwa kutengenezwa

“Tausi Aids Fund nilianzisha Ujerumani na ilifanikiwa kufanya kazi na foundation za Tanzania kama Wamata kipindi cha nyuma na kutoa michango. Pia nilifanya Dar es Salaam. Baada ya kuhama Ujerumani niliendelea kusaidia wenye ualbino kwenye shule za wasichana na hata nilitengeneza ‘Tv show’ kuelimisha,” amesema Likokola.

Amesema katika jitihada zake za kuisaidia jamii amekuwa akiungwa mkono na Serikali hali inayofanya aendelee kuisaidia jamii na kuweka nguvu zaidi katika eneo hilo.

“Miaka ya nyuma hata mabalozi wetu Ujerumani na Marekani walinishika mkono sana juhudi zangu, na kila nilipokuwa narudi Tanzania, pia serikali walinitambua na kunipa sapoti,” amesema Likokola.

Amesema ameanza tena kushughulika na mambo machache na kwamba kupitia atakayofanya ana imani ya kuungwa mkono na serikali.

Tausi ambaye alikuzwa katika ulimwengu wa mitindo miaka ya 90 alifanya kazi na kampuni za mitindo kama Gucci, Christian Dior, Issey Miyake, Tommy Hilfger, Escada. Pia aliandika majarida mengi ya mitindo na kuwavutia wanamitindo wengi wa sasa wa Kitanzania na wengine kote ulimwenguni.

Mwanamitindo mwenye watoto wawili anayeishi Marekani, mara kadhaa amekuwa akirejea Tanzania kufanya kazi katika miradi kadhaa sambamba na kusaidia wenye wananchi hasa wasichana kwenye miradi tofauti.

Tausi pia anajishughulisha na biashara ya kahawa kati ya Marekani na Tanzania, mwandishi wa vitabu vitabu na mtengenezaji wa maudhui ya televisheni.