TCB, Bunge wafungua ukurasa mpya kuinua wajasiriamali

DAR ES SALAAM: Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo, amemtembelea na kuzungumza na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na chombo hicho cha kutunga sheria.

Katika ziara hiyo iliyofungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya taasisi hiyo ya fedha na mhimili wa Bunge, Mihayo aliambatana na Mkurugenzi wa Biashara za Wateja Wadogo na wa Kati wa benki hiyo, Lilian Mtali,

Mazungumzo na kiongozi huyo wa Bunge linaloundwa na wabunge 393 kutoka majimbo 239 yalijikita katika masuala nyeti yanayohusu majimbo mbalimbali katika jitihada za kuendelea kuwainua wajasiriamali wadogo na wa kati.

Wawili hao walitambua mchango mkubwa wa kundi hili katika ukuaji uchumi na uzalishaji wa ajira mpya, mazungumzo yao yamejikita katika mpango wa utoaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa wajasiriamali.

Miradi hii itasaidia kukuza na kuchochea mazingira ya biashara kwa wajasiriamali pamoja na biashara zao.

“Lengo letu sio kutoa jibu moja kwa nchi nzima. Huwezi kuwa na suluhisho moja kwa watu wote, ndiyo maana ni muhimu kuwasikiliza wadau wengi iwezekanavyo. Njia hii itatusaidia kutoa majibu yatakayokidhi mahitaji ya wajasiriamali kulingana maeneo wanayoishi hata wale walioko vijijini,” alisema Mihayo.

Naye Dk Tulia Ackson alibainisha umuhimu wa ushirikiano huo na kusisitiza wajibu wa Bunge katika kutunga sera zinazowezesha maendeleo ya wajasiriamali na kuhakikisha kwamba biashara zao zinapata rasilimali zinazohitajika ili kukua.

PIA SOMA: TCB yajivunia mafanikio mradi wa SGR

“Maendeleo ya wajasiriamali ni muhimu kwa ukuaji uchumi wa taifa letu, kupitia ushirikiano huu na Benki ya TCB, tunaweza kutengeneza mazingira yatakayowezesha ukuaji wa biashara,“ amesema.

Kikao hicho kilihitimishwa kwa azimio la ushirikiano wa pamoja na kuendelea kubuni nyanja mbalimbali za ushirikiano lengo likiwa kuwainua wajasiriamali.

Habari Zifananazo

Back to top button