MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewasihi watumiaji wa huduma za mawasiliano kutumia msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka kuhakiki laini zao za simu, ili kujilinda na uhalifu mtandaoni.
Akizungumza kwenye kipindi cha runinga cha Morning Trumpet kinachorushwa na kituo cha Azam, Meneja wa Kitengo cha Usimamizi wa Huduma za Mawasiliano ya Simu na Intaneti wa Mamlaka hiyo, Sadath Kalolo alisema uhakiki wa laini za simu utawasaidia wananchi hasa watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu na intaneti kuwa salama.
“Unapohakiki laini zako za simu unajiweka salama wewe na watumiaji wengine wa mawasiliano, kwa kuwa wale wasiosajili laini wanazotumia kwa utambulisho wao watakosa huduma kwa kuwa ukizifuta namba hizo, zinafungwa,” alisisitiza.
Alielekeza jinsi ya kufanya uhakiki ambapo mtumiaji anapaswa kubofya nyota, kisha 106 na alama ya reli na kisha kufuata maelekezo.
Maelekezo hayo ni kuangalia usajili, kujua namba zilizosajiliwa katika mtandao mmoja, namba zilizosajiliwa mitandao yote, kufuta usajili na kuhakiki au kuongeza namba.
“Lengo ni kuangalia iwapo usajili wa laini umefanyika kwa usahihi, kuhakiki iwapo unatambua laini zote zilizosajiliwa kwa kutumia namba yako ya kitambulisho cha taifa na urasimishaji namba unazomiliki kwa kuitambulisha namba kuu na namba za ziada,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa mtumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu mara anapobaini uwepo wa namba ngeni kwenye orodha ya menyu ya uhakiki anapaswa kuifuta mara moja, kwa kuwasiliana na mtoa huduma wa mtandao anaotumia kupitia namba 100 au kufika kwenye duka la mtoa huduma au wakala wa mtoa huduma wa mtandao wake.
Kalolo alisema zoezi la kuhakiki na kuhamasisha uhakiki lilianza Desemba Mosi mwaka huu na litaendelea hadi Januari 30, 2023 na kwamba mara baada ya zoezi la kampeni ya uhamasishaji kukamilika watumiaji ambao namba zao za simu hazitakuwa zimehakikiwa kwa utambulisho wa kitambulisho cha uraia, zitafungwa.
Kuhusu watumiaji ambao walisajiliwa laini za simu na watu wengine kwa sababu mbalimbali zikiwemo kutokidhi vigezo vya umri au kukosa namba ya kitambulisho cha uraia na hivyo kusajiliwa na wazazi, walezi, ndugu, jamaa na rafiki, TCRA ilielekeza wahakikishe wanapata namba ya kitambulisho cha uraia kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kusajili laini hizo kwa utambulisho wao.
I don’t think the title of your article matches the content lol. Just kidding, mainly because I had some doubts after reading the article.