TCRA yaonya wasafirishaji vifurushi wasiosajiliwa

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa onyo kwa wasafirishaji vipeto na vifurushi ni kwa waliosajiliwa pekee huku ikitoa tahadhari kwa wateja wanaotumia huduma hizo kwa lengo la kuepuka hasara.

Ovyo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa tathmini ya kampeni inayoendelea nchini yenye lengo la kukabiliana na changamoto zinazokabili watumiaji wa huduma za usafirishaji hizo.

Alifafanua kuwa leseni kwa watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi na vipeto zinaongeza uwajibikaji wa watoa huduma kwa wananchi wanaowahudumia.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, kampeni hiyo ya elimu kwa umma inalenga kuwahamasisha wananchi kutumia watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi walioidhinishwa na kusajiliwa rasmi, ambazo zina ofisi zilizo rasmi, stoo za kuhifadhia vipeto na vifurushi, na rekodi nzuri ya ufanisi, usalama, na uadilifu katika utoaji huduma za kusafirisha vipeto na vifurushi.

“Usafirishaji wa vipeto na vifurushi unatembeza shughuli zetu za uchumi, sisi kama Mamlaka ya Mawasiliano sekta ya Posta ni sehemu ya eneo letu la usimamizi, hivyo tunao wajibu wa kuwakumbusha watoa huduma waliopo na wanaotoa huduma za kiposta au zinazohusiana na huduma za posta kama usafirishaji vifurushi na vipeto kuhakikisha wanasajili huduma zao hapa TCRA na wale ambao leseni zao zimefikia ukomo wahuishe leseni hizo,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu Bakari aliwakumbusha watoa huduma za usafirishaji vifurushi na vipeto yakiwemo mabasi ya abiria kwamba kufanya kazi za usafirishaji vifurushi na vipeto bila leseni ni kutenda kinyume na utaratibu wa sheria.

Kwa mujibu wa utaratibu wa TCRA, watoa huduma hiyo wanapaswa kusajili shughuli hizo kwa kutuma maombi ya kusajiliwa kupitia lango la watoa huduma za mawasiliano la TCRA linalopatikana mtandaoni kupitia ukurasa wa Tanzanite Portal unaomwezesha mwombaji kutolazimika kufika Ofisi za TCRA.

“Tumeboresha sana huduma zetu waombaji leseni zote za Mawasiliano wanaweza kupata leseni hizo kwa njia ya lango la Tanzanite,” alisisitiza.

TCRA inatoa leseni kwa kampuni za posta na usafirishaji wa mizigo katika makundi sita, ikiwa ni pamoja na kimataifa, Afrika Mashariki, ndani ya jiji, na kati ya majiji.

Katika kampeni hiyo ya miezi minne iliyoanza Machi, mwaka huu, watumiaji huduma za usafirishaji vipeto na vifurushi watapewa elimu kuhusu hatari za kutumia huduma za watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi na vipeto wasio na leseni ya TCRA; pia, watapewa Elimu kuhusu haki zao kama watumiaji kuhakikisha zinazingatiwa.

Haki za watumiaji wa huduma za kiposta ni pamoja na kupata taarifa kabla na baada ya huduma kushughulikiwa kwa malalamiko na kupata nafasi ya kukata rufani kwa Mdhibiti, miongoni mwa mengine.

Takwimu za hivi karibuni zilizochapishwa na TCRA zinaonyesha ongezeko la usafirishaji wa vifurushi na vipeto nchini Tanzania kutokana na ukuaji wa biashara mtandaoni. TCRA ilisisitiza watumiaji kuhakikisha wanajiridhisha na uhalali wa huduma za watoa huduma wanaowachagua kuwapatia huduma.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Alfa
Alfa
5 months ago

Tatizo baadhi ya hao waliosajliwa kusafirisha vifurushi bei zao ziko juu sana ,UKIRITIMBA na hawana Good customer care nzuri, hawazingatii muda, ndyo maana tunaenda na utaratibu wetu wa kienyeji mpaka hayo mapungufu wajirekebishe.Haiwezekani kusafirisha TV ya 30″ iwe Tshs30k au zaidi wakati jamaa zetu husafirisha kwa Tsh10k mpk TSh20,Nikikiwa na computer 20pc nikaomba kusafilishiwa ktk kampuni fulani iliyosajiliwa nikaambiwa nizipeleke ofisi kwao na kila pc watanicharge Tsh30k kwa Dar to Mtwara,Nikipowaona watu wa malory walifuata Mzigo ma kuniCharge Tsh20K kwa pc na mzigo unaupata Ontime bila mbambamba, hii ni ushindani kibiashara, Trust,value for money and customer and integrity, Siyo SIASA na kutoa matamko, tuwe wazi tubadilike tujenge nchi, Dunia yaenda kasi sana na mabadiliko ni mengi lkn sisi tumelala.
God bless Tanzania

Back to top button
1
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x