‘Tembeleeni banda letu mjue kanuni zao la kahawa’
WAKULIMA wa kahawa mkoni Kagera wameshauriwa kutembelea Banda la Utafiti wa zao la Kahawa (TACRI) katika maonesho ya Nanenane mkoani Kagera, ili kupata ujuzi wa kanuni bora za kilimo.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Sima kwa Niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatuma Mwasa, alitembelea banda hilo na kujionea namna wataalamu wa utafiti wa zao la kahawa wanavyotoa elimu ya kanuni bora za kilimo cha kahawa na namna ya kutambua magonjwa yanayoshambulia zao la kahawa kuelekea msimu wa kupanda zao hilo.
Amesema kuwa Mkoa wa Kagera unazalisha kahawa kwa wingi, lakini magonjwa mbalimbali yamekuwa yakishambulia zao la kahawa, hivyo wataalamu wa utafiti wanao wajibu wa kuhakikisha maonesho ya Nanenane yanakuwa chachu kwa wananchi kupata elimu sahihi ya kuwasaidia.
Ofisa Ugani na Mafunzo wa TACRI, Aretas Urassa alisema kuwa katika maonesho hayo wanaendelea kutoa elimu ya kanuni bora za kilimo kwa vitendo, kwani wana mashamba mengi katika viwanja vya Nanenane ya kujifunza kwa vitendo.
Amesema wakulima wote wanaopata fursa ya kutembelea banda lao wanapata elimu ya kilimo cha kahawa na wanafundishwa namna ya kutambua magonjwa yanayoshambulia kahawa na jinsi ya kuyatokomeza wao wenyewe.
Amesema kuwa taasisi hiyo mpaka sasa imetoa elimu kwa Wilaya za Missenyi na Kyerwa, zilizopo mpakani kuhusu ugonjwa wa bungua unaoshambulia kahawa.
Meneja wa ya Bodi Kahawa mkoani Kagera, Edmond Zani amesema kuwa kutolewa kwa elimu ya kilimo cha kahawa na mshikamano wa wadau kumechochea kupanda kwa takwimu za uzalishaji wa kahawa mkoani Kagera, ambapo msimu wa kahawa kwa mwaka 2022/2023 tani za kahawa zimefika 77,000 ukilinganisha na tani 52,000 kwa mwaka 2020/2021, ambapo matarajio ni kufikia tani 100,000 ifikapo mwaka 2025/2026.