TET yapata mwarobaini wa somo la Hesabu

TAASISI ya Elimu Tanzania (TET), imeingia makubaliano ya miaka mitatu na Chuo Kikuu cha Shanghai cha nchini China.

 Makubaliano hayo ni ya  kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa somo la hesabu ikiwemo mbinu wanazotumia kwa walimu pamoja na kufanya utafiti.
Akizungumza leo Machi 30,2023 jijini Dar es salaam, mara baada ya utiaji saini hati za makubaliano kati ya TET na Chuo hicho, Mkurugenzi Mkuu TET, Dkt. Aneth Komba amesema makubaliano hayo ya utafiti yatalenga kwenye somo la hesabu kutokana na changamoto za somo hilo kutofanya vizuri kwa kipindi kirefu hivyo kuwa mwarobaini kwani Shanghai ndiyo inaongoza kwa kutoa walimu na wanafunzi bora wa somo la hesabu Duniani.

Amesema, baada ya makubaliano hayo wanatarajia kupata namna nzuri ya kufundisha hesabu ikiwemo kupata mbinu za kuweza kuwavutia wanafunzi kujifunza somo hilo.
Aidha, amesema kuwa wamekubaliana baada ya mwaka mmoja kuongeza masomo mengine ambapo watafanya kwanza utafiti ili kujua wapi kunahitaji kushirikiana na chuo hicho kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo hayo.
“Kwa kuanza utafiti watakaoufanya utajikita zaidi kwenye somo la hesabu ikiwemo kufahamu changamoto na mbinu zipi bora kutumika katika mazingira ya Tanzania ambapo tafiti hizo zitajikita kwenye hatua ya shule za Msingi na Sekondari”. Amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo ya Mitaala, Dkt Fika Mwakabungu amesema mradi huo utatoa motisha kwa walimu kutokana na kupewa njia sahihi za kuwafundisha wanafunzi hapa nchini.
Amesema, utafiti waliofanya wamegundua wenzetu wa Shanghai wametuzidi kwenye masuala ya teknolojia hususani kwenye ufundishaji wa somo la Hesabu.

Naye Mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Shanghai amesema kuwa wataendelea kushirikisha na Taasisi ya elimu Tanzania (TET), katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo mbalimbali hapa nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button