SERIKALI imeipa mtaji wa shilingi bilioni 6 Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) ili isambaze mbolea ya ruzuku nchi nzima.
Taarifa hiyo imetolewa leo Januari 27, 2023 Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alipokuwa akizindua zoezi la usambazaji wa mbolea za ruzuku za TFC.
“Ni zaidi ya miaka nane sasa imepita tangu TFC mara ya mwisho wasambaze mbolea kwa wakulima. Pongezi kubwa kwa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan. “Amesema Mavunde
Amesema, serikali inatambua umuhimu wa TFC na inafahamu kuna mtandao mkubwa na madhubuti wa usambazaji wa mbolea nchini hivyo ni matarajio ya serikali kuwa itakwenda kuutumia vizuri kufikisha mbolea hizi za ruzuku kwa wakati kwa wakulima wote nchini.
“Mbolea si tu ni muhimu kwa wakulima katika kuongeza tija ya uzalishaji, bali pia ni mhimili mkubwa wa kuhakikisha nchi inazalisha zaidi na kuwa na uhakika na usalama wa chakula.” Amesema Mavunde na kuitaka Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TFC kufanya kazi kwa uweledi na uadilifu mkubwa.
Amesema serikali imeanza utekelezaji wa miradi mikubwa nchi nzima ili kuwezesha sekta ya Kilimo kukua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, miradi hiyo ikiwemo na ujenzi wa Mabwawa mapya 14 ya umwagiliaji ambayo yatahifadhi maji takribani lita Bilioni 131 na kuhudumia zaidi ya hekta 90,000.
Awali, akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi,, Meneja Mkuu wa TFC Samuel Mshote aliishukuru serikali kwa kuipa mtaji TFC na kuahidi kuwa yeye na timu yake watasimamia ipasavyo mtaji huo ili waweze kufikia matarajio makubwa ya serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo alipongeza hatua zilizochukuliwa na serikali za kuifufua TFC na kuipa mtaji ianze kufanya biashara, na kuongeza kuwa TFRA ipo tayari kuendelea kutoa miongozo thabiti ya Udhibiti ili TFC iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.