WAKALA wa Huduma za Misitu (TFS) imewataka watanzania kujifunza kutumia sumu ya nyuki kama njia mbadala ya kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukizwa na yasiyoambukizwa.
Mhifadhi Mwandamizi wa TFS kutoka shamba la miti Silayo wilayani Geita, Juma Mdoe amesema hayo wakati akitoa elimu katika maonesho ya saba ya teknolojia ya madini mjini Geita.
Mdoe amesema utafiti unaonyesha sumu ya nyuki ina mchanganyiko wa kampaundi tofauti ambazo zikiingia mwilini mwa binadamu husaidia kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya vimelea vya magonjwa.
“Sumu ya nyuki ikikuiingia cha kwanza kabisa inasisimua mfumo wa kinga ya mwili, kwa maana inaamusha na kupandisha kinga yako ya mwili, ambapo ikipanda inasaidia kupambana na maradhi,” amesema.
SOMA: Hifadhi ya Kigosi rasmi chini ya TFS
Amedokeza kuwa, sumu ya nyuki imethibitika kisayansi kuwa na uwezo wa kusaidia kuondoa matatizo ya uvimbe mwilini na pia ina viambata vya collagen ambayo ni muhimu katika kuboresha afya ya ngozi.
“Sambamba na hilo pia sumu ya nyuki ina kompaundi ambazo ziko imara katika kupambana na virusi ama maradhi mbalimbali ya virusi, tena vile virusi sugu vya maradhi makubwa,” amesema.
Ameeleza kwa kutambua umuhimu huo wa sumu ya nyuki TFS wamekuja na huduma ya kudungisha chanjo ya sumu ya nyuki mmoja au wawili kwa watu walio tayari ili kuimarisha kinga za mwili.
Mdoe amewatahadharisha watanzania kuacha kutojiingiza kwenye matumizi holela ya sumu ya nyuki bali wanapaswa kufuata taratibu na miongozi ili kuepuka madhara ya kiafya ya sumu ya nyuki.
Aidha amesema kuwa TFS inaendelea na ujenzi wa viwanda vya mazao ya nyuki ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/25 wamejipanga kujenga kiwanda kipya katika shamba la miti silayo wilayani Geita.
Mnufaika wa chanjo ya Sumu ya Nyuki, Lissa Richard amesema tangu apatiwe elimu hiyo amevutiwa na aina hiyo ya tiba mbadala na kuahidi kutembelea mara kwa mara ofisi za TFS kupata huduma hiyo.
Kwa upande wake Peris Bogo amekiri tangu apate elimu ya udungwaji wa nyuki ameipanga kuwa endelevu kwani maumivu ya kungatwa na nyuki hayaofautiani na kuchomwa sindano.