THRDC yaomba suluhu ya mgogoro wa kanisa la ufufuo

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umetoa wito kwa serikali kutatua hali ya sintofahamu inayoendelea kulikumba Kanisa la Ufufuo na Uzima, likisisitiza kuwa waumini wa dhehebu hilo wana haki ya kufanya ibada kama inavyotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mratibu Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema kuwa licha ya kutokuwepo kwa tamko rasmi la kulifungia Kanisa hilo, bado waumini wake wamewekwa njia panda kutokana na hali ya kutoeleweka iliyoibuka.
“Hatuwezi kusema kama Kanisa hili limefungiwa au halijafungiwa, kwa sababu kwa mujibu wa barua ya Waziri na maamuzi ya mahakama za chini, hakuna ufafanuzi ulio wazi. Hali hii imewaweka maelfu ya waumini wake katika sintofahamu,” amesema Wakili Olengurumwa.
Aidha, amebainisha kuwa Askofu Amos kutoka Shinyanga, pamoja na baadhi ya waumini waliowakilisha maelfu ya waumini wa Kanisa hilo nchini, waliwasiliana na THRDC ili kutafuta msaada wa kutetea haki yao ya msingi ya kuabudu.
SOMA ZAIDI: THRDC: Polisi boresheni utaratibu wananchi kuingia mahakamani
“Tunafarijika kuona kwamba watu wakiwa na changamoto, wanatutambua kama wadau muhimu wa kutafuta suluhu. Tumekuwa tukishiriki kwenye majadiliano ya maridhiano kwa muda mrefu, na sasa tunaombwa kuwa sauti ya wale ambao haki zao zinakandamizwa,” ameongeza.
Olengurumwa amewataka viongozi wakuu wa serikali akiwemo Waziri Bashungwa, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), na Kamanda wa Kanda Maalum Muliro, kuhakikisha kuwa haki za waumini hao zinalindwa kwa kuruhusu waumini wa Kanisa hilo kufanya ibada wakati mgogoro wa taasisi yao ukiendelea kushughulikiwa.
“Watanzania hawajafungiwa kuabudu. Kinacholalamikiwa ni taasisi, lakini watu binafsi bado wana haki ya kuabudu kila Jumapili kama Wakristo wengine wote,” amesema.
Ameongeza kuwa licha ya barua ya wizara kueleza kuwa hakuna agizo la kufungia Kanisa hilo, bado makao makuu ya Kanisa hilo yanaendelea kulindwa na askari polisi, hali inayozua maswali zaidi kuhusu uhuru wa kuabudu kwa waumini wake.
THRDC imesisitiza kuwa haki ya kuabudu ni ya kikatiba na imetoa wito kwa serikali kutatua suala hili ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima na kulinda misingi ya haki za binadamu nchini.