SERIKALI kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika kipindi cha miaka 10, jumla ya miradi 4,543 ilisajiliwa yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 53.1 na kutoa ajira ya watu 654,260.
Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mufindi Kusini, David Kihanzile (CCM) bungeni jijini hapa jana.
Kihenzile alitaka kufahamu kwa miaka 10 ni wawekezaji wangapi wa nje walionesha nia ya kuwekeza na wangapi walifanikiwa.
“Kupitia TIC, jumla ya miradi 4,543 ilisajiliwa katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2021 ambapo mitaji yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 53.1 ilitarajiwa kuwekezwa na kutoa ajira 654,260,” alisema Naibu Waziri.
Alisema kati ya miradi hiyo, miradi 3,304 ilitekelezwa sawa na asilimia 72.7 ya miradi yote iliyosajiliwa.
Kigahe alisema serikali imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kufanikisha uwekezaji ikiwamo kuimarisha matumizi ya Tehama, dirisha moja la kuhudumia wawekezaji, kuboresha na kujenga miundombinu wezeshi, vivutio (vya kikodi na visivyo vya kikodi) na kutenga maeneo kwa ajili ya wawekezaji.
Aidha, amesema wizara hiyo inaratibu utekelezaji wa mifuko na programu 62 za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Ngara, Ndaisaba Ruhoro (CCM) na kuongeza kuwa serikali imekamilisha tathmini ya mifuko na Programu za Uwezeshaji 20.
Kigahe alisema serikali inafanyia uchambuzi taarifa ya tathmini hiyo na kuja na hatua za kuchukua ili kuboresha utoaji wa huduma wa mifuko husika.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Oliver Semguruka (CCM), Kigahe alisema wizara kupitia Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) inataka kukopesha wajasiriamali viwanda au teknolojia rahisi badala ya kuwapa fedha ili kuzalisha bidhaa katika viwanda hivyo vidogo ili kukidhi mahitaji ya mikopo waliyoomba.
Akijibu swali la Mbunge wa Momba, Condesta Sichalwe (CCM), alisema serikali inaangalia namna ya kuzisaidia halmashauri ambazo hazina uwezo wa kukidhi mahitaji ya vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu vinavyohitaji mikopo.