TIC yatoa huduma kwa miradi 1,038
KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetoa huduma zinazotakiwa kwa miradi 1,038 ya wawekezaji sawa na asilimia 81.7 kati ya miradi 1,270 iliyoisajili katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2018 hadi 2022.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri katika ripoti ya uwekezaji ya kila mwezi ya kituo hicho kwa Machi mwaka huu. Teri alisema mafanikio hayo yalichangiwa na ushirikiano uliopo kati ya wadau wakiwamo wawekezaji na kituo katika kushughulikia changamoto mbalimbali ikiwamo ya upatikanaji wa vibali, uidhinishaji, ardhi, leseni na masuala ya kodi.
“Serikali itaendelea kuhakikisha mazingira ya biashara na uwekezaji yanaboreshwa ili kuvutia zaidi uwekezaji wa ndani na wa nje,” alisema Teri. Kwa mujibu wa Teri, katika kipindi cha Machi mwaka huu, TIC ilitoa huduma kwa miradi 1,247 ya wawekezaji ikiwamo kuitembelea ikilinganishwa na huduma iliyotolewa kwa miradi 122 Februari mwaka huu.
Alisema ongezeko hilo la utoaji huduma kwa miradi lilitokana na jitihada za TIC katika kufuatilia na kutathmini ufanisi wa miradi hiyo.
Teri alisema katika mwezi uliopita, TIC ilitembelea miradi 25 ikilinganishwa na miradi mitano Februari, kupiga simu za ufuatiliaji kwa miradi 1,202 ikilinganishwa na miradi 114 Februari pamoja na kufanya ziara ya kufuatilia utekelezaji kwa miradi 20 iliyopewa hati ya ardhi ikilinganishwa na miradi mitatu Februari mwaka huu.