Tido asimulia Charles Hillary alivyopenda kufanya naye kazi

MWANAHABARI mkongwe, Tido Mhando amesema uwezo wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Charles Hilary ulimfanya atake kufanya naye kazi.

Tido alisema hayo wakati wa kuaga mwili wa Charles katika Viwanja vya Mapinduzi Square mjini Unguja jana.

Alisema yeye ndiye aliyemshawishi, Charles atoke Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW) kwenda Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na baadaye Azam Media nchini kutokana na uwezo wake.

Alieleza kuwa mwaka 1980 wakati, Charles anajiunga na Radio Tanzania, yeye alikuwa ameshaondoka miezi sita kabla na akiwa Nairobi, Kenya alianza kusikia sauti nzuri ya kijana mgeni ambaye alivutiwa nayo.

Tido alisema aliporudi Dar es Salaam alikutana naye na kumueleza alivyovutiwa na sauti yake na Charles alimueleza yeye (Tido) ni kati ya watu waliomfanya aipende kazi ya utangazaji.

“Baadaye akahamia Redio One bado tukawa tunawasiliana na baadaye akaenda DW wakati huo mimi nipo BBC na nilikuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili. Katika mabadiliko ya haraka haraka tulitaka kutangaza mpira wa Uingereza kwa sababu nilitaka kuhakikisha tunakuwa na mtangazaji mzuri… kichwani mwangu alikuja Charles, lakini alikuwa tayari DW,” alisema Tido.

Alisema alimpigia simu aende London kujiunga na BBC akakubali na mchakato wa kumtoa DW kwenda BBC ulikuwa mgumu.

“Tukakubaliana tufanye siri akawa anakuja hadi London anatafuta kisingizio kazini na mimi kwa kuwa nilikuwa najua akijulikana siri ingetoka, akawa anakuja kwangu sehemu za kufanya usaili nilikuwa namfanyia utaratibu apitie taratibu zote akamaliza akafaulu,” alisema Tido.

Alisema baadaye alimshawishi arudi nyumbani akafanye kazi Kampuni ya Azam Media na alikubali, lakini alimweleza azungumze na mkewe.

“Charles akaja Azam watu wengi walishangaa na hata viongozi wa Azam walikuwa hawaamini na kiukweli kuja kwake ndio ukawa mwanzo wa chachu kubwa sana ya maendeleo Azam,” alisema Tido.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema kifo cha Charles ni kama mbuyu ulioanguka.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maofisa Habari na Mawasiliano wa Serikali Zanzibar, Raya Hamad Suleiman alisema Charles alikuwa mlezi wao.

Mwanahabari mkongwe, Farouk Karim alisema Charles alikuwa daraja kati ya wanahabari wa Zanzibar na serikali.

Imeandikwa na Lidya Inda na Zena Chande.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button