‘Timiza Fund imekuwa chachu ya mafanikio’

DAR ES SALAAMM; Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Zan Securities Limited, Raphael Masumbuko, amesema uwekezaji wa pamoja umeanza kuwa chachu ya kuwainua kiuchumi Watanzania wengi.
Amesema hatua hiyo inatokana na mafanikio makubwa ambayo Timiza Fund imeyapata kwa kuwa na ongezeko kubwa la wawekezaji na thamani ya mfuko tangu ulipoanzishwa mwaka 2024.
Ameeleza kuwa Zan Securities Limited ilisajiliwa rasmi Oktoba mwaka 2009 ikiwa na timu ya watu wawili tu. Hata hivyo Safari ya Mafanikio, baada ya miaka 14 ya kazi na uwekezaji katika rasilimali watu, kampuni hiyo sasa ina wataalamu zaidi ya 25 waliobobea katika sekta ya masoko ya mitaji.
Amesema Mei, 2024 kampuni hiyo iliandika historia kwa kuwa wakala wa kwanza wa Soko la Hisa nchini kuzindua Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja ulioidhinishwa na CMSA.
“Lengo lilikuwa moja tu kuwapa Watanzania wa vipato vyote nafasi ya kuanza safari ya ustawi wa kifedha kupitia uwekezaji unaosimamiwa kitaalam,” amesema Masumbuko
Amesema tangu uzinduzi wake Mei, 2024 yanaonyesha mafanikio makubwa, ambapo katika mauzo ya awali walilenga kukusanya Sh bilioni 10, lakini waliweza kupata Sh bilioni 10.38, sawa na asilimia 103.8 ya lengo.
Amesema thamani ya mfuko imeongezeka kutoka Sh bilioni 10.38 Julai 2024 hadi kufikia Sh bilioni 31.7 Machi 4, 2026, ikiwa ni ukuaji wa zaidi ya asilimia 200 tangu kuanzishwa kwake.
Kwa upande wa idadi ya wawekezaji, amesema mfuko ulianza na wawekezaji 210 mwezi Julai 2024 lakini hadi sasa umefikia wawekezaji 8,741, ongezeko la zaidi ya asilimia 4,000 ndani ya kipindi cha takribani miaka miwili.
Vilevile, thamani ya kipande cha uwekezaji imeongezeka kutoka Sh 100 hadi Sh 131.78 kufikia Machi 4, 2026.
“Awali tulianza na ukuaji wa asilimia 13.5 kwa mwaka, lakini sasa tumefikia asilimia 15 kwa mwaka kutokana na utaalamu katika kuchagua maeneo bora ya uwekezaji ili kuhakikisha mwekezaji anapata faida zaidi,” amefafanua Masumbuko
Katika hatua nyingine, Masumbuko amesema kampuni imeanzisha Zan Investment App ambayo inaleta mapinduzi ya kidijitali katika sekta ya uwekezaji nchini kwa kurahisisha huduma kwa njia ya kidijitali.
Kupitia programu hiyo, wawekezaji wanaweza kuwekeza na kufuatilia salio lao popote walipo nchini kwa kutumia simu zao za mkononi.
Amesema matumizi ya teknolojia pia yamesaidia kupunguza gharama za uendeshaji na hivyo kuongeza thamani ya faida kwa wawekezaji huku wakipata taarifa za uwekezaji wao kwa wakati halisi.
Amesema uwekezaji wa pamoja ni nyenzo muhimu katika kujenga uchumi imara na kuongeza ushiriki wa wananchi katika huduma za kifedha.
“Tafiti zinaonyesha kuwa maendeleo ya nchi yanaendana moja kwa moja na matumizi ya huduma za kifedha. Kupitia Timiza Fund, tunajenga utamaduni wa uwekezaji kwa kila Mtanzania,” amesema.



