MASHINDANO ya Mei Mosi ya Kitaifa mwaka huu yamepangwa kuanza Aprili 16, 2023 katika viwanja tofauti mkoani Morogoro kwa kushirikisha timu zaidi ya 24 kutoka taasisi za serikali, mashirika ya umma na taasisi zisizo za kiserikali.
Mashindano hayo yatazinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa, Aprili 20, 2023.
Mjumbe wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi Kitaifa , Twaibu Dowile amesema hayo Aprili 15, 2023 kwa niaba ya Katibu wa Kamati ya Mashindano Kitaifa Taifa , Moshi Makuka baada ya kukamilika kwa upangaji wa ratiba ya michezo mbalimbali itakayofanyika hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu.
Dowile amesema michezo utakaofanyika leo ni kwa upande wa mpira wa miguu kwa kuzikutanisha timu ya Kilimo dhidi ya Afya na mchezo wa pili ni baina ya TRA na CRDB na michezo hiyo inafanyika kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro .
“ Matarajio yetu ya kuzindua michezo hii ni Aprili 20, mwaka huu ambapo tunatarajia mgeni rasmi atakuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro,Fatma Mwassa” amesema Dowile.
Amesema ratiba hiyo itaendelea siku inayofuatia kulingana na timu zilizopangwa katika makundi yao ambapo mchezo wa soka una makundi manne yenye timu nne hadi tano na kwenye mchezo wa netiboli pia kuna makundi manne yenye timu tatu hadi nne .
Dowile ametaja michezo mingine mbali ya soka na Netiboli ni kuvuta kamba ,mbio za baiskeli ,riadha, michezo ya jadi ambayo ni Bao ,Drafti , Karata na Volleyboll ambao unachezwa kwa mara kwanza katika mshindano ya Mei Mosi ya mwaka huu.
Makundi yaliyopangwa kwa upande wa soka ,kundi A lina timu za Tamisemi, Mahakama , Kilimo, Mawasiliano na Afya , kundi B lina timu za TRA, SUA , CRDB, TPDC na Tanroads , kundi C lina timu ya Ulinzi , Hazina Ushirika na Mambo ya Ndani wakati kundi D likiwa na timu ya Maliasili , Uchukuzi , Utumishi na Tanesco .
Kwa upande wa Netiboli kundi A lina timu Uchukuzi, Ushirika , Halmashauri ya wilaya ya Gairo, na TRA, kundi B lina timu ya Mambo ya Ndani, CRBD, Ulinzi na Tanroads , kundi C lina timu ya Ikulu, Afya , Utumishi na TPDC wakati kundi D likiwa na timu ya Tanesco, Mahakama , Maliasili na Mawasiliano.
Michezo huo licha ya kufanyika katika uwanja Jamhuri Morogoro , vingine ni SUA, Morogoro Sekondari, Ujenzi ,Tumbaku na Mazimbu .