TIRA yabainisha magari yanavyokwamisha ukataji bima

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima (TIRA) imesema magari chakavu yanayotaka kukatiwa bima imekuwa kikwazo kwa taasisi hiyo katika kukubaliana na matakwa ya wamiliki wa magari hayo kukatiwa bima.

Kamishna wa TIRA, Dk. Baghayo Saqware ametoa kauli hiyo katika mkutano na watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma akitoa elimu ya umuhimu wa bima kwa jamii kwa ajili ya kuhamasisha ukataji wa bima za mali,afya na vyombo vya moto.

Saqware amesema wamekuwa wakipata wakati mgumu kukubali kuyakatia bima baadhi ya magari ambayo yamekuwa na uchakavu mkubwa ambayo kwa mujibu wa sheria na taratibu za bima hazikidhi vigezo vya kukatiwa bima.

Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi Bima wa Kanda ya Ziwa Tanganyika, Kulenje Mbura pamoja na hilo  amewahamasisha viongozi na wananchi wa Mkoa Kigoma kuwekeza zaidi katika uanzishaji wa ofisi zinazotoa huduma za bima kwani mkoa wa kigoma bado uko nyuma kwa wananchi wake kukata bima licha ya kuwa na biashara nyingi na kubwa zinazopaswa kukatiwa bima.

Akifungua mkutano huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa amewataka watendaji katika ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Kigoma kutumia elimu ya umuhimu wa bima walioipata kuiepeleka kwa jamii ili  kubadili mtazamo wa  jamii katika kutambua umuhimu wa bima na kukata bima mbalimbali kwa ajili ya maisha yao.

Sambamba na hilo Katibu Tawala huyo wa Kigoma ameitaka TIRA kufanya mapitio ili kujua kuna uhitaji kiasi gani ili serikali ya mkoa iongeze nguvu katika kuhakikisha jamii ya mkoa wa Kigoma inafikiwa na elimu ya bima ili waweze kuokoa maisha ya watu na mali zao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button