TIRA yahimizwa kufanya kazi kidigitali

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande.

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imezindua taarifa ya utendaji wa soko la bima huku ikihimizwa kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuhakikisha inafanya kazi kidigitali ili kwenda sambamba na kasi ya ukuaji.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa taarifa hiyo ya mwaka 2023 Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande amesema sekta ya bima ina jukumu la kuhakikisha inasaidia kujenga uchumi na kuwapa wananchi ulinzi imara wa afya zao.

Kamishna wa Bima Tanzania, Dk Baghayo Saqware.

Amesema hivi karibuni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya ‘Bima ya Afya’ kwa wote ambayo kwa namna moja au nyingine inalenga kuona kila Mtanzania anakuwa na bima hiyo,  hatua ambayo inapaswa kuchangamkiwa na kila mmoja.

Advertisement

SOMA: TIRA yatoa maelekezo kuepuka udanganyifu

“Tafiti na tathmini mbalimbali zinaonesha soko la bima linakuwa kila siku na taswira ya uzinduzi wa mwaka huu inaonesha wazi soko hilo litaendelea kukua zaidi hivyo ni wakati muafaka kwa TIRA kujipanga kuhakikisha inaenda sambamba na ukuaji, muwe mstari wa mbele kuhamasisha uwekezaji, na kuhakikisha sekta ya bima inaendelea kuimarika maradufu,”amesema.

Kamishna wa Bima Dk Baghayo Saqware amesema ukuaji huo umechagizwa na serikali kwa kuweka mazingira mazuri na kutoa maelelekezo ambayo yamesababisha soko kukua.

Ametaja viashiria vya ukuaji ni pamoja na kuongezeka kwa ada za bima kwa asilimia 7.4 kutoka sh bilioni 1.155 hadi sh bilioni 2.023 huku uandikishaji wa bima mtawanyo ukiongezeka kwa asilimia 30.4 kutoka sh bilioni 201.3 mwaka 2022 hadi bilioni 262.5 kwa mwaka 2023.

Pia, amesema ajira katika sekta za bima zimeongezeka kwa asilimia 34.1 kutoka 4173 mwaka 2022 hadi 5595. Mali za uwekezaji zikiongezeka kwa asilimia 26.8 kutoka sh bilioni 1.697 mwaka 2022 hadi 2.152 mwaka 2023.

Amesema mchango wa sekta ya bima kwenye Pato la Taifa umeongezeka kwa asilimia 2.01 kwa mwaka 2023 kutoka asilimia 1.99 kwa mwaka 2022.

Pia, madai ya bima yanayolipwa yameongezeka kwa asilimia 25.5 kutoka sh milioni 389 mwaka 2022 hadi milioni 488.2 kwa mwaka 2023 huku madeni yakiongezeka kwa asilimia 44.4 kutoka sh bilioni 1.007 hadi sh bilioni 1.45 na ubakizaji wa bima za kawaida ukiongezeka kwa asilimia 12.3.