TISEZA yaridhishwa uwekezaji kiwanda cha vifungashio

KAGERA: Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetembelea kiwanda cha kuzalisha vifungashio cha L&N Standard Packaging Solution chenye uwekezaji wa Sh bilioni 6 na kulidhishwa na hatua ya kiwanda hicho ambacho kitasaidia kupunguza uagizaji wa vifungashio kutoka nje nchi.
Ziara ya TISEZA katika mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani na kuanzisha viwanda na kuongeza thaman mazao ya kilimo na kuchochea ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa ambayo imeanzishwa mwaka 2024.

Mwenyekiti wa TISEZA, Balozi Aziz Mlima amesema kuwa watanzania wanapaswa kubadili mtizamo juu ya swala la uwekezaji kwa sababu hakuna mbadala wa nchi yao ,hivyo serikali imepunguza masharti kwenye uwekezaji na uagizaji wa mitambo hivyo ni vyema Watanzania kuchangamkia Fursa ya uwekezaji na kuunganishwa katika mfumo ya kifedha.
“Tunajihusisha na kutoa elimu kwa wawekezaji wa ndani hii nchi ni ya kwao ,wakiwekeza serikali inawaunaunganisha na mifumo ya kifedha ,lakini pia Kuna ushuru unapunguzwa katika uagizaji wa mitambo lengo ni kufanya viwanda vyetu vifanye kazi kwetu na tupate bidhaa kutoka kwetu ajira zitapatikana na mzunguko fedha utaongezeka,”amesema Mlima.

Alitoa wito kwa Watanzania wenye uwezo kupunguza woga katika maswala ya uwekezaji kwani kwa sasa kinachotakiwa ni kuwa na eneo la uwekezaji ,hati ya kiwanja ,Mali zisizohamishika na pesa kidogo ya kuanzia, andiko zuri la mradi, kujisajili TISEZA na baada ya hapo serikali itakuunganisha na mifumo ya fedha ili ufanye uwekezaji.
Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Batreth Jacobo akitoa taarifa ya uwekezaji kwa timu ya TISEZA amesema kuwa anaishukuru serikali na viongozi kwa kuwapa moyo wa kuwekeza kwani kwa sasa kiwanda hicho kinapokea oda nyingi za vifungashio kutoka mikoa mbalimbali na wako hatua za mwisho za kuuza vifungashio hivyo nje ya nchi.

Amesema kiwanda hicho pia kimefanikiwa kutoa ajira kwa vijana na wanawake 57 na wameunganishwa katika taasisi za fedha kupata mkopo ili kufanya uwekezaji mkubwa.



