TLS: Aliyewazuia polisi mahakamani si wakili

TLS: Aliyewazuia polisi mahakamani si wakili

CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimesema Baraka Mkama aliyejitambulisha kama wakili na kuonekana akiwazuia polisi wasiwatie nguvuni wateja wake baada ya kuachiwa huru mahakamani, si wakili wala wala mwanachama wa TLS.

Rais wa TLS Wakili Harold Sungusia pamoja na Baraza la uongozi la TLS, wametoa taarifa rasmi leo kuhusiana na  tukio lililotokea Mei 23, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, ambapo Mkama alionekana akiwazuia askari polisi wasiwatie nguvuni wateja wake baada ya kuachiwa huru na mahakama.

Kwa mujibu wa Sungusia baada ya kupokea taarifa za tukio hilo, Baraza la Uongozi la TLS walifanya kikao cha dharura na kuunda Kuunda Kamati Teule ya uchunguzi, ambayo ilipewa hadidu za rejea za kufanya uchunguzi wa haraka wa wakitaalam wa tukio hilo, kisha kuujulisha uongozi wa TLS kwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Advertisement

Amesema kamati hiyo ya watu wanne ikiongozwa naa Mwenyekiti wa TLS Tawi la Ilala, ilianza kazi yake Mei 24, 2023 na kukamilisha taarifa yake Mei 26 na ilifanikiwa kumhoji Mkama na kisha mazungumzo na Jeshi la Polisi, uongozi wa mahakama na baadhi ya mawakilio waliokuwa na taarifa ya tukio hilo.

Amesema pia kamati ilipitia mfumo wa usajili wa mawakili ili kujiridhisha kuhusu taarifa za Mkama, ambapo amesema wakati kamati ikimhoji Mkama alikiri yeye sio wakili ingawa amekuwa akifanya kazi kama wakili tangu mwaka 2019 na kwamba katika mashauri aliyokuwa anayasimamia akiigiza kama wakili alikuwa akiwatoza wateja wake Sh milioni tatu.

Amesema Kamati Teule iliwasilisha taarifa ya uchunguzi wa tukio hilo la Baraza la Uongozi wa TLS, ambapo baraza lilipitia na kujadili na kujiridhisha kuwa Mkama sio wakili wala mwanachama wa TLS.

“Mawakili rasmi na halali ni lazima awe mwanachama wa TLS, pia yupo katika mfumo wa e – wakili kwa wanaotumia simu janja(smartphone) kupitia mfumo tambuzi  wa mawakili unaoitwa e-wakili. ukiingiza jina la wakili inakuletea picha na details zake, kama sio wakili haitakuletea picha wala details,” alisema Rais wa TLS, Sungusia.

Amesema TLS itashirikiana na vyombo vya dola na vyombo vya utoaji haki, ili kuhakikisha kuwa hatua stahiki za kisheria zinachukuliwa dhidi ya Mkama pamoja na watu wengine wenye tabia kama hizo.

“Tumepokea simu nyingi kutoka mikoa mbalimbali, tayari wametupa taarifa muhimu za ziada kuhusu mtandao wa watu wasiokuwa mawakili wanaofanya kazi za uwakili(vishoka), hivyo tunaipa muda Kamati Teule ya uchunguzi kuendelea kufuatilia mtandao huo na kuwasilisha taarifa zake za ziada ifikapo tarehe 31 Mei 2023, ” alisema Sungusia.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *