MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema inafuatilia mifumo ya hali ya hewa kuhusu kunyesha kwa mvua za El Nino baada ya kuonesha kuwa mpaka sasa kuna uwezekano wa kunyesha mvua hizo kwa asilimia 60.
Hatua hiyo inatokana na taarifa ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) iliyoeleza kunyesha kwa mvua hizo nyingi katika nchi za Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika, Mashariki ya mbali na Amerika ya Kati.
Mvua hizo ambazo zimekuwa zikinyesha kila baada ya miaka miwili na kwa mara ya mwisho nchini zilinyesha mwaka 2016 na kusababisha madhara yakiwemo mafuriko.
Kaimu Meneja Ofisi Kuu ya Utabiri TMA, Dk Mafuru Biseke alisema kwa sasa mifumo ya hali ya hewa inaonesha joto la Bahari ya Pasifiki kuongezeka katika eneo la kati na kuonesha uwezekano wa kunyesha kwa mvua hizo kwa asilimia 60.
“Kwa sasa tunaelekea kipindi cha mwezi Juni mpaka Septemba ambao ni kipindi cha kipupwe kinachoambatana na upepo mkali na kipindi cha ukavu,” alisema Biseke.
Alisema uwepo wa El Nino kutokea unategemea na kukubaliana kwa mifumo iliyopo sasa na mingine na iwapo itanyesha kwa mvua za El Nino zitanyesha katika maeneo ya Kaskazini mwa nchi, Pwani ya Kaskazini katika mikoa ya Pwani, Kaskazini mwa mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Tangana visiwa na Unguja.
Pia katika Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na ukanda wa Ziwa Victoria katika mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Simiyu na Kagera.
Taarifa ya TMA kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa ilifuatilia mifumo ya hali ya hewa wakati wa maandalizi ya msimu wa mvua za masika (Machi hadi Mei) mwaka huu na inaendelea kufuatilia mifumo hiyo ikiwemo El Nino.
Taarifa hiyo kuhusu ufafanuzi juu ya uwepo wa hali ya El Nino na uhusiano wake katika mienendo ya mvua nchini ilieleza kuwa El Nino ni mfumo wa hali ya hewa unaosababishwa na uwepo wa joto la bahari la juu ya wastani katika eneo la kati la kitropiki la Bahari ya Pasifiki.