TMA yapongezwa utendaji kazi

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imepongezwa kwa uboreshwaji wa utabiri wa hali ya hewa na taarifa za tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa nchini.

Mwakilishi wa Katibu Tawala wa mkoa wa Morogoro, Dk Rozalia Rwegasira ametoa pongezi hiyo kwa niaba ya serikali ya mkoa wakati wa ufunguzi wa Semina ya Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Jamii Kukabiliana na Athari za mabadiliko ya hali ya hewa na matukio ya hali mbaya ya hewa, kwa ajili ya kupunguza hasara na uharibifu

Dk Rozalia ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya uchumi na uzalishaji wa mkoa huo Morogoro amesema utabiri wa hali ya hewa umeendelea kuboreshwa na tahadhari za mvua kubwa na matukio ya hali mbaya ya hewa zinatolewa kwa wakati na mamlaka hiyo.

Amesema kutolewa kwa wakati wa utabiri huo kumechangia kuokoa maisha ya watu na mali zao ,na pia utekelezwaji wa mradi huo utakuwa na faida kubwa na chanya kwa wananchi wa Tanzania.

Dk Rozalia aliipongeza serikali kwa kupitia TMA kwa kazi hiyo njema na kwamba mkoa wa Morogoro inaahidi kushirikiana na TMA katika kufanikisha utekelezwaji wa mradi huo.

“Kwa niaba ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa tuanaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika na taarifa zitakazozalishwa na TMA kupitia Mradi huu, ili wadau na wananchi waweze kuchukua tahadhari kwa lengo la kupunguza athari zitokanazo na matukio ya hali mbaya ya hewa,”amesema Dk Rozalia.

 

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Hali ya Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dk Ladislaus Chang’a ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya hali ya hewa nchini.

“Nitumie fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa Serikali kwa kuendelea kuwekeza na kuisaidia TMA katika kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini kwa kuweka sera, mikakati na mazingira wezeshi yanachochea ubunifu na umahiri”amesema Dk Chang’a.

Dk Chang’a alisisitiza kwamba uwekezaji wa serikali kwenye miundombinu ya hali ya hewa nchini ndio chanzo kikuu cha uboreshwaji wa taarifa za hali ya hewa nchini .

Pia ametoa shukrani za dhati kwa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kufadhili mradi huu muhimu ambao utaongeza ufanisi katika mchakato wa kukabiliana na mabadiliako ya hali ya hewa na tabianchi nchini.

Mbali na hayo amewasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari zinazotolewa na TMA, na pia kuzingatia sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa namba 2 ya mwaka 2019 na kanuni zake.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button