TNBC yajivunia mafanikio Serikali ya Samia

BARAZA la Taifa la Biashara (TNBC) limesema Serikali ya Awamu ya Sita imeboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji.

 

Katibu Mtendaji wa TNBC, Dk Godwill Wanga amesema kumekuwa na maboresho yakiwamo ya sera kuondoa tozo na ukiritimba uliokuwa unakwamisha ustawi wa biashara na uwekezaji nchini.

Alisema hayo Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ambayo TNBC imepata.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu, Rais Samia Suluhu Hassan ameifungua nchi kiuchumi ikiwemo kuimarika kwa ushirikiano na uhusiano kati ya sekta binafsi na umma. Imetekeleza pia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Mkumbi) ili kuvutia uwekezaji na kukuza biashara nchini.

Dk Wanga alisema kwa kuongozwa na Rais Samia, TNBC imeimarisha mabaraza ya biashara ya mikoa na mabaraza ya biashara ya wilaya na imetatua changamoto zilizowakabili wafanyabiashara.

 

“Lengo la kuanzisha mabaraza hayo katika ngazi ya mikoa na wilaya ni kuwezesha serikali za mitaa kushughulikia changamoto za biashara na uwekezaji katika halmashauri pale ambapo kuna mwingiliano wa mara kwa mara na wafanyabiashara,” alisema Dk Wanga.

 

Alisema serikali imeondoa tozo na makato hivyo kupunguza gharama za kufanya biashara nchini na kuongeza thamani katika bidhaa zinazozalishwa.

 

“Tumeweza kupiga hatua kubwa katika kuvutia uwekezaji nchini kwani tumekuwa tukifanya maboresho mbalimbali ikiwemo kuondoa tozo na makato na hivyo kuwezesha kampuni kujitengenezea faida na kukuza mitaji yao,” alisema Dk Wanga.

 

Alisema nchi imepiga hatua kuimarisha na kuhamasisha matumizi ya kidijiti na hivyo kuchangia kukuza uchumi kwa kuongeza mapato ya serikali.

 

Katibu mtendaji huyo alisema nchi imeendelea kuimarisha na kutekeleza kwa vitendo sera na sheria ya diplomasia ya uchumi na matokeo yamekuwa yakionekana kupitia uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi za nje.

Habari Zifananazo

Back to top button