Tozeni gharama stahiki huduma za afya – Dk. Harold

DAR ES SALAAM: WATOAJI wa huduma za afya nchini wametakiwa kutoza gharama stahiki za huduma ya afya ili kumsaidia Mtanzania kupata huduma kwa urahisi kupitia bima zao za afya pia kuhakikisha dhamira ya serikali kuidhinisha bima ya afya kwa wote inafikiwa kwa wepesi na haraka.

Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jubilee Insurance (Bima ya Afya), Dk. Harold Adamson amesema serikali imeweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuwa wabunifu na wenye maono ili kumfikia mwananchi wa hali ya chini.

SOMA: Serikali: Bima ya Afya kwa wote itarahisisha huduma

“Unaweza kuona tuna bima ambayo mtu anaweza kulipa hata Sh. 300 kwa mwezi,” amesema Harold na kuongeza kuwa wamezindua kampeni ya ‘Kuna kuishi na kuna kuishi huru. There’s living and there’s living free’,” amesema ofisa huyo.

, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jubilee Insurance (Bima ya Afya), Dk. Harold Adamson

Amesema hatua ya serikali kupitisha bima ya afya kwa wote linaendana na kuongeza uelewa wa bima kwa wananchi kwani takwimu zinaonesha uelewa kuhusu bima ni chini ya asilimia moja.

“Kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuchochea watanzania wenzetu kujiunga na bima afya na bima ya maisha,” amesema Adamson.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jubilee Insurance (Bima ya Maisha), Helena Mzena amesema dhana ya bima ni ya watu fulani sio sahihi badala yake bima ya afya humsaidia mtu yeyote kupata huduma ya afya wakati wote.

“Wote kwa mfano, tuna ugua haijalishi mkubwa au mdogo. Kwahiyo ni muhimu kujua bima inakusaidia wakati unayo au huna fedha mkononi,” amesema Mzena.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jubilee Insurance (Bima ya Maisha), Helena Mzena akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam

Pia, amesema kampeni ya ‘Kuna kuishi na kuna kuishi huru’ ina lengo la kuwafanya watanzania kuishi huru na kuwa na amani ya moyo kwa kuwa na bima bora ya afya inayopatikana kirahisi kwa njia ya kidijitali.

Aidha, kwa pamoja taasisi hiyo wameipongeza Wizara ya Afya kwa kushirikiana na taasisi binafsi ikiwemo taasisi za bima katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili kuhakikisha uhakika na usalama wa maisha ya Mtanzania katika shughuli zake za kila siku.

Pia wamesifu maamuzi ya Rais Samia Suluhu Hassan kusaini muswada wa bima ya afya kwa wote kuwa sheria ambayo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha 2024-25.

Habari Zifananazo

Back to top button