DODOMA: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameagiza Bodi na Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuja na mpango wa muda mrefu utakaoonesha jinsi nchi itakavyoweza kuongeza kiasi cha gesi asilia ili muda wote kuwe na hazina ya kutosha ya nishati hiyo inayotumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme, viwandani, majumbani na katika magari.
Dk. Biteko ameyasema hayo Novemba 21, 2023 alipokuwa kwenye kikao na Bodi na Menejimenti ya TPDC ambacho kililenga kufahamiana, kubadilishana mawazo juu ya utendaji kazi ambapo Dk. Doto Biteko amewaelekeza matarajio ambayo nchi inayahitaji kutoka TPDC.
“TPDC tujiulize, Je uwezo wetu wa kuzalisha Gesi Asilia unaweza kujibu mahitaji yetu ya Gesi ? tujiulize hili na tuchukue hatua. Tutambue kuwa mahitaji ya Gesi Asilia ni makubwa kwa sasa kwani dunia inahama kutoka matumizi ya mafuta na kwenda kwenye Gesi Asilia hivyo lazima tujipange, na pia tukumbuke tumesaini makubaliano ya kusafirisha nishati hii kwenda Uganda, Zambia na Kenya hivyo lazima tuwe na Gesi ya kutosha.” Amesema Dk. Biteko.
Amesema amewataka TPDC kutokuwa na urasimu katika uchukuaji wa maamuzi mbalimbali ikiwemo kwenye shughuli za utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia ili kutorudisha nyuma sekta hiyo nchini.
Kuhusu maelekezo aliyoyatoa wakati wa ziara yake, katika Kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi na Kijiji cha Madimba na Msimbati mkoani Mtwara, Dk. Biteko amesisitiza kuwa, maisha ya wananchi katika maeneo hayo ambayo kuna visima na mitambo ya Gesi Asilia lazima yabadilike na wapewe huduma bora ikiwemo maji, umeme, afya na usafiri.
“Nashukuru mmeanza kufanyia kazi maagizo niliyoyatoa kwa haraka, ikiwemo ya kuweka taa za barabarani Kijiji cha Msimbati, kupeleka umeme wa uhakika Madimba na Msimbati unaotoka kwenye mitambo ya Gesi Asilia, kupeleka kivuko kisiwa cha Songosongo na malipo ya mafao kwa wastaafu wa Knight Support ambao walikuwa wakilinda mitambo na visima vya Gesi Asilia Songosongo ambao hawakulipwa muda mrefu, watu hawa wanahitaji huduma bora.” amesema Dk. Biteko
Katika Hatua nyingine, Dk. Biteko ameiagiza TPDC kupita kwenye Halmashauri zote nchini zinazopokea ushuru wa huduma kutokana na shughuli za Mafuta na Gesi Asilia kufanyika kwenye Halmashauri hizo ili TDPC ijihakikishie kwamba, fedha hizo zinaenda pia kwenye vijiji/maeneo ambayo shughuli za uzalishaji wa Gesi Asilia zinafanyika.