TPDC yarejesha kwa jamii mali ya milioni 64/-

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesaidia jamii zilizo pembezoni mwa bomba la gesi asilia kwa kuwajengea wodi ya mama na mtoto pamoja na ofi si ya serikali ya mtaa kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni 64.

Miradi hiyo imefanyika katika Kijiji cha Mwanambaya, Kata ya Mipeko, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani walipojenga wodi ya mama na mtoto katika Zahanati ya Mwanambaya iliyokamilika kwa gharama ya Sh milioni 53.3 kati ya hizo TPDC ilitoa milioni 50 na serikali ya kijiji ikitoa milioni tatu na zaidi.

Pia katika Mtaa wa Kiponza Kata ya Chamanzi, Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam wamesaidia ujenzi wa ofisi ya serikali ya mtaa kwa gharama ya Sh milioni 14. Wakikabidhi miradi hiyo juzi, TPDC ilisema fedha hizo zimetolewa ikiwa ni mkakati wake kurejesha kwa jamii zilizopo karibu na miradi yao ikiwa ni kutambua umuhimu wa wananchi hao kwa kuwa walinzi wa miradi hiyo muhimu kwa serikali.

Ofisa Maendeleo ya jamii wa TPDC, Delian Kabwogi akikabidhi miradi hiyo alisema kuna vijiji na mitaa zaidi ya 139 iliyo pembezoni mwa bomba la gesi katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani mpaka Dar es Salaam na wamekuwa wakisaidia katika sekta mbalimbali za afya, elimu, utawala bora, michezo na nyinginezo.

Alisema katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 jijini Dar es Salaam kwa mwaka huu wamesaidia miradi mitatu Shule ya Msingi Mzambarauni ya watoto wa mahitaji maalumu Sh milioni 69, ujenzi wa ofisi ya serikali ya mtaa ya Kiponza Sh milioni 14 na ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Mtaa Ulongoni A, Sh milioni nane.

Aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuendelea kuwa walinzi wa miundombinu ya bomba la gesi asilia kwa kuhakikisha hakuna nayefanya shughuli za kilimo, uchimbaji mchanga, biashara au kuchoma moto juu ya miundombinu hiyo kwa ajili ya usalama wa bomba na wananchi wa maeneo hayo.

“Naomba kila mmoja akawe balozi wetu wa kulinda miundombinu ya bomba la gesi asilia na unapobaini tatizo kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali za mitaa na tunafuraha kuwa fedha tulizotoa zimetumika kama ilivyotarajiwa,” alisema.

Akikabidhi wodi ya wanawake na watoto katika zahanati ya Mwanambaya, Kabwogi alitaka uongozi wa Wilaya ya Mkuranga kukamilisha vifaa vinavyotakiwa ili wodi hiyo ianze kufanya kazi kwani ujenzi umekamilika kwa asilimia 100.

Akipokea wodi hiyo, Katibu wa Afya wa Wilaya ya Mkuranga, Salma Mhiko alisema wodi hiyo siyo msaada kwa kijiji hicho chenye wakazi 9,248 pekee bali kwa halmashauri yote kutokana na zahanati kutumika na watu wa vijiji vingi vinavyopakana na kijiji hicho cha Mwanambaya.

Akimwakilisha Mganga Mkuu wa Wilaya alisema zahanati hiyo inahudumia wagonjwa wa nje zaidi ya 1,200 kwa mwezi hivyo wodi hiyo itasaidia akinamama kujifungua kwa usiri na kulinda utu wao kutokana na kuwa na eneo zuri la kujifungua.

Akisoma risala ya Mtaa wa Kiponza, Kata ya Chamanzi Wilaya ya Temeke waliojengewa ofisi ya serikali ya mtaa, Mjumbe wa serikali ya mtaa, Fauthia Shakiri alisema ofisi hiyo imejengwa kwa Sh milioni 14.2 lakini bado haijakamilika na wanahitaji Sh milioni 10.1 kukamilisha ujenzi na samani za ofisi.

Habari Zifananazo

Back to top button