TPF-NET yatua wodi ya waliojifungua Katoro

GEITA: Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF-NET) mkoa wa Geita umetembelea na kutoa zawadi kwa kina mama waliojifungua katika wodi ya wanawake iliyopo kituo cha afya Katoro wilayani Geita.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polis (SACP) Safia Jongo ameongoza ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.

Kamanda Jongo amesema dhamira kuu ya tendo hilo la hiari na majitoleo ni kuwashika mkono kina mama na kuwatia moyo kwa kila hatua wanayopitia katika kufanikisha uzazi salama.

Amesema hatua hiyo pia inalenga kuikumbusha jamii, mbali ya kuwa askari polisi ni watumishi wa umma lakini pia na wao ni wazazi na wanatambua thamani ya mwanamke katika jamii.

“Mbali ya kuwa sisi ni askari polisi lakini pia sisi ni wanawake, na pia tunataka kuithibishia jamii kwamba kuwa sisi askari haimaaniishi uanawake wetu haupo”, amesema Kamanda Jongo.

Kamanda Jongo ametaja baadhi ya msaada waliotoa ni mashuka pamoja vifaa vya usafi ili kuwezesha wanawake wajawazito na wale wanaojifungua kusalia katika sehemu safi na salama.

“Tunaendelea kutoa rai kwa jamii kumthamini mwanamke, matendo ya ukatili wa kijinsia na watoto wa kike yameendelea kuwepo, licha ya kuwa tunajitahidi kutoa elimu.

“Nitoe wito kwa jamii kwamba ukatili ni kosa la jinai na adhabu yake ni kali, tuendelee kuwathamnini wanawake’, amesisitiza Kamanda Jongo.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Katoro, Dkt Yohana Kitutu amekiri kuwa msaada wa TPF-NET mkoa wa Geita utasaidia kuongeza akiba ya mashuka na vifaa vya usafi kwa mahitaji ya ziada.

Amekiri kuwa kituo cha afya Katoro kina wanawake wengi wanaojifungua kiasi cha wastani wa watoto 700 kila mwezi hali inayoashiria ongezeko la mahitaji ya vifaa vya wodini.

Kaimu Mwenyekiti Kitongoji cha Katoro-Center, Paul Sanane amesema msaada huo unachochea ushirikiano wa jamii na polisi na kusaidia kupunguza matukio hususani ukatili katika familia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button