TPHPA yaagizwa kudhibiti viuatilifu visivyo na viwango

ARUSHA: MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeagizwa kudhibiti shehena za vipando vinavyoingia nchini ili kuzuia baadhi ya mimea yenye changamoto ya magonjwa inayoweza kuleta athari kwa wakulima ikiwemo viuatilifu visivyo na viwango.
Aidha, katika kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo kupitia uongozi bora wa Rais Samia katika kuhakikisha usalama wa chakula unaimarika nchini serikali imewezesha TPHPA kununua ndege yenye thamani ya Sh bilioni 6 kwa ajili ya kuangamiza ndege aina ya kweleakwelea ambao wamekuwa hatarishi kwenye mazao ya nafaka nchini.

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikiaUshirika na Umwagiliaji, Dk, Stephen Nindi kwaniaba na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati wa kilele cha maadhimisho ya Kimataifa cha Siku ya Afya ya Mimea yenye kauli mbiu ya “Umuhimu wa Afya ya Mimea katika Afya Moja”yenye mchango mkubwa katika utoshelevu wa chakula kwa asilimia 128.

Amesema endapo udhibiti wa magonjwa hayo ukimarishwa utawezesha wakulima kunufaika na mimea yenye tija zaidi sanjari na kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya kilimo kinacholeta tija kubwa kwa watanzania hususan wanawake ambao wanamchango mkubwa katika mnyororo mzima wa chakula kupitia afya ya mimea.

Naye Mkurugenzi wa TPHPA, Profesa, Joseph Ndunguru amesema katika kudhibiti baa la panya TPHPA imefanya udhibiti huo katika mikoa 16 ,wilaya 54 na kata 540 na kuokoa jumla ya ekari 358,895 za mazao ikiwemo mahindi, udhibit wa ndege aina kwelea katika halmashari 24 na kuokoa zaidi ya tani 110,000 ikiwemo mpunga uwele na mtama.



