TPSA yaomba msaada wa Sh milioni 15.6

DAR ES SALAAM : CHAMA cha Kuogelea kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania (TPSA) kimetoa ombi la msaada wa Sh milioni 15.65 ili kufanikisha Mashindano ya Tatu ya Taifa ya Utambuzi wa Vipaji, yatakayofanyika Oktoba 11, 2025 katika bwawa la kuogelea la Shule ya Sekondari Shaaban Robert, Upanga, Dar es Salaam.

Mashindano hayo yamelenga kutambua na kukuza vipaji vya waogeleaji wenye ulemavu wa viungo, macho, akili na ulemavu wa aina nyingine, sambamba na kuendeleza ujuzi wao na kujenga timu ya taifa itakayoshiriki mashindano ya kimataifa, ikiwemo Michezo ya Paralympic itakayofanyika Los Angeles mwaka 2028.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TPSA, Ramadhan Namkoveka alisema mchango wa kifedha au vifaa kutoka kwa wadau wa michezo, makampuni, taasisi na watu binafsi utasaidia kuboresha mashindano na kuinua mchezo wa kuogelea kwa watu wenye ulemavu nchini. “Tunawaalika wadau wote kujitokeza kusaidia kifedha au vifaa. Mchango wowote utasaidia kuboresha mashindano na kuendeleza mchezo wa kuogelea kwa watu wenye ulemavu nchini,” alisema Namkoveka.

Aidha, TPSA imewataka waogeleaji kutoka mikoa yote nchini kujiandikisha kushiriki, ambapo dirisha la usajili litafungwa Septemba 29, 2025. SOMA: Kuogelea wapo imara michezo Afrika

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button